Dar es Salaam.
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kijitonyama sasa wana nafasi zaidi ya kujifunza, kufanya majaribio na kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia baada ya Airtel Africa Foundation kuzindua upya jengo la Airtel Fursa Lab lililokarabatiwa.
Airtel Fursa Lab, iliyoanzishwa mwaka 2020 kwa ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), imekuwa kituo cha kujifunzia na kukuza ujuzi wa kidijitali kwa wanafunzi, walimu na vijana kutoka ndani na nje ya jamii inayozunguka shule hiyo.
Ukarabati wa jengo la Airtel Fursa Lab umeongeza mazingira ya kujifunzia na kufanya majaribio, huku kituo hicho kikilenga kuwawezesha vijana kutumia teknolojia kwa ajili ya kujifunza na kubuni suluhisho za changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya watu 5,800 wamenufaika na Fursa Lab, wakiwemo wanafunzi, walimu, vijana, wajasiriamali na wanawake.
Kituo hicho pia kimekuwa kikitoa fursa kwa wanafunzi waliomaliza Darasa la Saba, Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na wahitimu wa vyuo vikuu kupata ujuzi wa kidijitali, biashara, ubunifu na stadi nyingine.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo lililokarabatiwa, Mkuu wa Programu kutoka Airtel Africa Foundation, Esi Prah, alisema uwekezaji huo una lengo la kuwapa vijana mazingira na zana za kuwawezesha kutumia teknolojia kwa vitendo.
“Tunaamini kuwa upatikanaji wa teknolojia na elimu ya kidijitali unaweza kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapatia maarifa, ujasiri na ujuzi wanaohitaji ili kutengeneza suluhu mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” alisema Prah.
Alisema Airtel Fursa Lab imejengwa katika dhana ya kuwapa vijana nafasi ya kujifunza na kujaribu mawazo yao.
Katika kituo hicho, wanafunzi hupata fursa ya kujifunza na kufanya mazoezi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Sayansi ya Kompyuta, programu za kompyuta, biashara, stadi za maisha, chakula na lishe ya binadamu, pamoja na ushonaji na ubunifu.
Airtel Fursa Lab pia imeunganisha wanafunzi na majukwaa ya kujifunzia kama ShuleDirect, Maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanznaia (TET) na WazoLearn, pamoja na maudhui yanayotokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI).
Kwa miaka kadhaa, kituo hicho kimekuwa pia sehemu ya kukuza vipaji na ubunifu kwa wanafunzi.
Wanafunzi walionufaika na Airtel Fursa Lab wameweza kushiriki katika programu mbalimbali na kuwa Mabalozi wa UNICEF na Plan International, wabunifu wa Oky, wasanii wa kidijitali na wabunifu katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
Miongoni mwa miradi iliyobuniwa na wanafunzi ni programu ya kufuatilia mzunguko wa hedhi iliyolenga kuwasaidia wasichana kupata taarifa na kufuatilia mzunguko wao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema Fursa Lab ni sehemu ya juhudi za kampuni kupanua fursa za elimu ya kidijitali kwa vijana nchini.
“Ukarabati na ufunguzi upya wa Airtel Fursa Lab unaakisi dhamira yetu ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata zana, maarifa na fursa wanazohitaji ili kufanikiwa katika dunia ya kidijitali,” alisema Singano.
Alisema lengo ni kuhakikisha teknolojia inatumika kama nyenzo ya elimu, ubunifu na kujenga fursa za kiuchumi, badala ya kubaki kuwa chombo cha mawasiliano pekee.
“Kupitia ushirikiano wetu, Airtel sasa imeunga mkono zaidi ya shule tano, na tutaendelea kufanya kazi na washirika wetu kuwafikia vijana na jamii nyingi zaidi,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kijitonyama, Bi. Halima Juma, alisema Airtel Fursa Lab imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya shule hiyo katika TEHAMA na ubunifu.
“Tunashukuru sana kwa uwekezaji huu kwa walimu wetu, wanafunzi na jamii kwa ujumla. Tangu mwaka 2020, Fursa Lab imewawezesha wanafunzi na walimu wetu kupata ujuzi wa kidijitali, mafunzo ya vitendo na fursa za ubunifu,” alisema.
Bi. Juma alisema kituo hicho kimepanua wigo wa shule kwa kuwapa vijana kutoka nje ya shule hiyo nafasi ya kupata maarifa na ujuzi wa kidijitali.
“Imefungua shule yetu kwa wanafunzi kutoka nje ya jamii yetu, na kuwapa maelfu ya vijana fursa ya kupata maarifa na elimu ya kidijitali,” alisema.
Alisema Airtel Fursa Lab pia imechangia kuboresha ujifunzaji wa TEHAMA na kuwasaidia wanafunzi kutumia teknolojia katika kutatua changamoto.
Matokeo hayo yanaonekana katika mafanikio ya shule hiyo, ambayo imeorodheshwa katika nafasi ya 10 kitaifa katika TEHAMA kwa miaka mitatu mfululizo.
Wanafunzi wake pia wameshinda tuzo tatu katika mashindano ya Girls in ICT, yanayolenga kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika teknolojia.
Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na Fursa Lab ni Angel Swai, ambaye amebuni suluhisho la taa za kuongozea magari linalotumia akili mnemba (AI).
Angel alisema kituo hicho kimemsaidia kwenda zaidi ya nadharia anayojifunza darasani na kupata nafasi ya kufanya majaribio ya mawazo yake.
“Airtel Fursa Lab imenipa nafasi ya kujifunza, kufanya majaribio na kubadilisha mawazo yangu kuwa kitu cha vitendo,” alisema.
Alisema mazingira na rasilimali zinazopatikana katika kituo hicho zimemsaidia kuona namna teknolojia inavyoweza kutumika kushughulikia changamoto halisi.
“Kupitia ujuzi na rasilimali zinazopatikana hapa, nimeweza kuchunguza namna teknolojia na AI zinavyoweza kutumika kushughulikia changamoto halisi katika jamii zetu,” alisema.
Kwa Angel, uzoefu huo unaonyesha umuhimu wa kuwapa vijana zana na mazingira ya kuendeleza mawazo yao.
“Ubunifu wangu ni mfano wa kile ambacho vijana wanaweza kufanikisha wanapopewa zana na fursa zinazofaa,” alisema.
Ukarabati wa Airtel Fursa Lab unatarajiwa kuendelea kutoa nafasi kwa wanafunzi, walimu na vijana wengine kujifunza ujuzi wa kidijitali, kufanya majaribio na kukuza ubunifu.
Shule ya Sekondari Kijitonyama imeishukuru Airtel Africa Foundation, Airtel Money, DTBi na Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono Airtel Fursa Lab na kuongeza fursa za elimu ya kidijitali kwa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...