BENKI ya AbsaTanzania na Kampuni ya Knauf Gypsum Tanzania zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuanzisha Mpango wa Ufadhili kwa Wasambazaji (Distributor Financing Programme), hatua inayolenga kuwawezesha wasambazaji wa Knauf kupata mitaji ya biashara kwa urahisi zaidi, kuimarisha mnyororo wa ugavi na kuchochea ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini.
Kupitia makubaliano hayo, Benki ya AbsaTanzania itatoa huduma maalum za kifedha kwa wasambazaji watakaokidhi vigezo vya benki, ikiwa ni pamoja na mikopo ya mtaji wa biashara na ufadhili wa ununuzi wa bidhaa. Awamu ya kwanza ya mpango huo inatarajiwa kuwahusisha wasambazaji kati ya 30 na 40 kutoka mtandao wa Knauf nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika makao makuu ya Knauf Gypsum Tanzania jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki AbsaTanzania, Bw. Obedi Laiser alisema, ushirikiano huo unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kutumia huduma za kifedha kuimarisha biashara na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa biashara.
"Ushirikiano huu unaonesha nguvu ya mfumo shirikishi wa huduma za kibenki katika kusaidia ukuaji wa biashara na kuleta manufaa kwa wadau wote. Kwa kuwapatia wasambazaji wa Knauf suluhisho za kifedha, tunawawezesha kuongeza uwezo wao wa biashara, kuboresha ufanisi na kutumia kikamilifu fursa za ukuaji. Absa tunaendelea kutekeleza dhamira yetu ya kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, hatua moja baada ya nyingine," alisema Bw. Laiser.
Alisema mpango huo utawapa wasambazaji uwezo wa kupata mitaji ya kuendesha biashara, kuongeza akiba ya bidhaa na kupanua shughuli zao, jambo litakaloimarisha upatikanaji wa bidhaa za Knauf katika soko la Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Knauf Gypsum Tanzania, Bw. Christoforos Stamoulakatos, alisema ushirikiano huo utawajengea uwezo wasambazaji wa kampuni hiyo na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja.
"Wasambazaji wetu ni sehemu muhimu ya mafanikio ya kampuni yetu na uwezo wetu wa kuwahudumia wateja kote nchini. Kupitia ushirikiano huu na Absa Bank Tanzania, tunawapa fursa ya kupata huduma za kifedha zitakazowasaidia kukuza biashara zao na kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka sokoni," alisema.
Mpango huo unaendana na mkakati wa Benki ya Absa Tanzania wa mfumo shirikishi wa huduma za kibenki unaolenga kutoa huduma jumuishi za kifedha zinazosaidia mnyororo mzima wa thamani kwa kuwaunganisha wazalishaji, wasambazaji na wadau wengine wa biashara kupitia suluhisho bunifu za kifedha.
Knauf Gypsum Tanzania ni mmoja wa wateja wakubwa wa Benki ya Absa Tanzania katika kitengo cha Wateja wa Makampuni (CIB), na kampuni hiyo imeendelea kuwa mdau muhimu katika sekta ya ujenzi nchini. Kupitia mpango huo mpya, taasisi hizo zinatarajia kuimarisha zaidi ushirikiano wao na kufungua fursa mpya za ukuaji wa biashara kwa wadau wote.
Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Benki ya Absa Tanzania na Knauf Gypsum Tanzania, wasambazaji, washirika wa biashara pamoja na wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw Obedi Laiser (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Knauf Gypsum Tanzania, Bw. Christoforos Stamoulakatos, wakisaini Hati za Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuanzisha Mpango wa Ufadhili kwa Wasambazaj, hatua inayolenga kuwawezesha wasambazaji wa Knauf kupata mitaji ya biashara kwa urahisi zaidi, kuimarisha mnyororo wa ugavi na kuchochea ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja wa Sheria na Mahusiano ya Nje na Serikali wa Knauf, Bi. Flora Erasto na kulia ni Katibu wa Kampuni kutoka Benki ya Absa Tanzania, Bw. Desmond Malyi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...