Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Idara ya Organizesheni, Paul Chacha amesema uongozi wake utasimamia uchaguzi wa haki na usawa ndani ya chama, akisisitiza kuwa hakuna mwanachama atakayepokonywa haki yake kutokana na ushawishi wa fedha au mamlaka ya watu binafsi.
Akizungumza katika makao makuu ya CCM jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, Chacha amesema CCM ndiyo chama kilichojipanga zaidi nchini na kinaendelea kuwahakikishia Watanzania amani, maendeleo na matumaini ya maisha bora.
Amesema uchaguzi ndani ya chama unapaswa kuwa wa haki na uwazi ili kumpata kiongozi anayestahili kwa ridhaa ya wanachama, huku akiahidi kusimama imara kulinda misingi ya demokrasia bila kuyumbishwa na shinikizo lolote.
Chacha ametoa onyo kwa watu wanaokusudia kutumia fedha kujinufaisha kisiasa, akisema ni heri fedha hizo zikaelekezwa kwenye uwekezaji au biashara kuliko kutumika kuwarubuni wapiga kura.
Aidha, amesisitiza kuwa CCM haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kununua kura au kushawishi wanachama kwa fedha ili kupata nafasi za uongozi, akibainisha kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaokiuka maadili ya chama.
Vilevile, amesema chama hakitasita kuwachukulia hatua watu wanaotumia nafasi au mamlaka ya ndugu zao kuingilia mchakato wa uchaguzi na kutoa maelekezo yanayokandamiza haki za wanachama.
Kwa mujibu wa Chacha, uchaguzi wa haki ndio msingi wa kupata viongozi wenye uwezo wa kukijenga chama na kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uwajibikaji.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...