Na Belinda Joseph – Dodoma

Walimu wenye ulemavu mkoani Dodoma wamepatiwa elimu ya fedha, uwekezaji na hifadhi ya jamii ili kuwajengea uwezo wa kusimamia kipato, kuwekeza na kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu, mafunzo hayo yameandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Elimu  Mkoa wa Dodoma Mwalimu Kiduma Mageni, wakati akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa, amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa watumishi kwa kuwa inawasaidia kupanga matumizi, kuweka akiba na kuwekeza, akisisitiza kuwa changamoto za kifedha haziwezi kutatuliwa kwa kuongeza kipato pekee bila kuwa na uelewa wa kukisimamia.

Mwalimu Kiduma amesema walimu wanapaswa kuanza kujiandaa kwa maisha ya baada ya kustaafu mapema kwa kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi, akiba na uwekezaji ili kuepuka changamoto za kifedha wanapomaliza utumishi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa CWT, Alfred Alexander, amesema mafunzo hayo yamelenga pia kuwaandaa walimu kukabiliana na maisha baada ya kustaafu, akieleza kuwa baadhi ya wastaafu wamekuwa wakipoteza mafao yao kutokana na kuingia kwenye uwekezaji bila kuwa na uelewa wa kutosha.

Alfred amesema CWT imeialika Mwalimu Commercial Bank kutoa elimu kuhusu fursa za kifedha na uwekezaji, ili kuwasaidia walimu kuanza uwekezaji wakiwa bado kazini na kujenga vyanzo vya ziada vya kipato.

Mkuu wa Idara inayohudumia Walimu Wenye Ulemavu wa CWT, Mwalimu Robert Bundala Katuba, amesema mafunzo hayo yamewapa walimu uelewa kuhusu mabadiliko ya sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na fursa za uwekezaji, huku akizitaka taasisi nyingine kuunga mkono juhudi za kuwawezesha walimu wenye ulemavu.

Mwalimu Robert amesema CWT inathamini ushirikiano na NSSF katika kutoa elimu hiyo na kwamba maarifa yanayopatikana yanapaswa kuwafikia walimu wengine pamoja na jamii, hususan kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kutumia fursa zinazopatikana.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Dodoma amesema mfuko huo utaendelea kushirikiana na CWT kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, akieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuwasaidia kuelewa huduma zinazotolewa na NSSF na fursa zinazopatikana kupitia hifadhi ya jamii.

Mafunzo hayo yameweka mkazo katika umuhimu wa walimu wenye ulemavu kuwa na uelewa wa fedha, uwekezaji na hifadhi ya jamii mapema, ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kujenga vyanzo vya ziada vya kipato na kuwa na maisha yenye utulivu wakati wa utumishi na baada ya kustaafu.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...