Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kutembelea Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ya Nane Nane ili kupata elimu kuhusu ulinzi wa amana zao na taratibu za kufidiwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Isack Kihwili, amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha wanaweka fedha zao katika benki na taasisi za fedha zilizosajiliwa na kupewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania.
Amesema kufanya hivyo ni muhimu kwa kuwa kuweka fedha katika taasisi zisizo rasmi kunaweza kuwanyima wananchi haki ya kupata fidia endapo taasisi hizo zitashindwa kutekeleza majukumu yake au kushindwa kurejesha fedha za wenye amana.
Kihwili pia amewataka wenye amana katika iliyokuwa Benki ya FBME ambao bado hawajachukua fedha zao kujitokeza haraka ili kukamilisha mchakato wa malipo, akisema fedha zao bado zinawasubiri.
Amesema DIB imefikia hatua kubwa katika kulipa madai ya wenye amana wa benki hiyo, huku akibainisha kuwa ni asilimia ndogo tu ya walengwa ambao bado hawajajitokeza kuchukua fedha zao.
Kwa mujibu wa Kihwili, madai ya wenye amana wa FBME kwa upande wa Tanzania yalifikia takribani Sh bilioni 35, ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 85 ya fedha hizo tayari zimelipwa kwa walengwa.
Amesema bado kuna takribani watu 428 ambao hawajajitokeza kuchukua fedha zao zenye thamani ya karibu Sh bilioni nne, licha ya fedha hizo kuwa tayari zimetengwa kwa ajili yao.
“Tunawasihi wale ambao bado hawajajitokeza kuchukua fedha zao wafanye hivyo haraka, kwa sababu fedha hizo zimetengwa na zipo tayari kwa ajili ya malipo,” amesema.
Amefafanua kuwa baada ya kundi hilo kujitokeza na kulipwa fedha zilizotengwa kwa ajili yao, hatua inayofuata itakuwa ni kulipa asilimia 15 iliyobaki ili kuhakikisha kila mwenye amana anayestahili fidia analipwa madai yake kwa asilimia 100, kwa kuzingatia taratibu zinazotumika.
Aidha, Kihwili amesema bado kuna kundi la wadai wengine, wakiwemo baadhi ya wafanyakazi waliokuwa na madai yaliyofikishwa mahakamani, ambao malipo yao hayajahusishwa katika awamu inayoendelea kutokana na mchakato wa kufuatilia na kuhakiki mali za benki hiyo.
Amesema DIB inaendelea kufuatilia mali zilizobaki za benki hiyo ili kuhakikisha fedha za kutosha zinapatikana na kuwezesha kukamilishwa kwa malipo ya wadai hao kwa kuzingatia taratibu za kisheria.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...