Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu taasisi za dini likiwemo kanisa Katoliki katika kuimarisha huduma za kijamii, maendeleo na ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa mchango wa taasisi za dini ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya Tanzania.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Jumapili, Agosti 30, 2026, katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Mpanda, yaliyofanyika mkoani Katavi, ambapo amesema Serikali inatambua mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za elimu, afya na huduma za kiroho.

“Serikali inatambua mchango wa Kanisa na baba Askofu. Kila tunapotaja maendeleo ya nchi yetu, kuanzia mwanzo mpaka hapa tulipofika, hatuwezi kuyataja kwa kina maendeleo hayo bila kutaja mchango wa Kanisa.”

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa umeendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha huduma za kijamii na shughuli za maendeleo zinaimarika, akisisitiza kuwa milango ya Serikali itaendelea kuwa wazi kwa Kanisa na taasisi nyingine za dini katika masuala yanayolenga ustawi wa wananchi.

“Niwahakikishie Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa na popote pale mlipo na jambo msisite, milango yetu iko wazi ili tuweze kuhakikisha kwamba tufanye jambo lolote linalotufurahisha.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa viongozi wa Mkoa wa Katavi na mamlaka husika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara, maji na umeme, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma hizo kwa wakati.

Amesema maandalizi ya kukabiliana na uwezekano wa kutokea kwa El Niño yanapaswa kwenda sambamba na hatua za vitendo, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa mifereji na madaraja ili kupunguza athari za mafuriko.

Kuhusu huduma za maji, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maji na wahusika wa mradi wa maji Mpanda kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ifikapo Desemba 2026, huku akisisitiza pia kuharakishwa kwa miradi ya barabara inayounganisha Katavi na mikoa jirani.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya haki kwa wananchi, akitangaza kuwa Serikali inaelekea kufuta sheria inayohusu utaifishaji wa mifugo, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto za wananchi kunyang’anywa mifugo yao.

“Katika Bunge hili linaloendelea tunakwenda kufuta sheria ya utaifishaji wa mifugo... kumekuwepo na majeraha makubwa ya watu kunyang’anywa katika baadhi ya maeneo. Tunataka tuondoe hayo ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaepukana na hayo.”

Pia ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa sheria kuacha kukamata vitendea kazi vya wananchi kama pikipiki, bajaji na magari katika utekelezaji wa sheria za makosa mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kutumia utaratibu wa kisheria wa adhabu na faini.

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Mhashamu Baba Askofu Eusebius Nzigilwa, amemshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda na kushiriki katika maadhimisho hayo, akisema uwepo wake umeonesha heshima na kuthaminiwa kwa Jimbo la Mpanda na Kanisa Katoliki Tanzania.

“Ninakushukuru sana. Tunaona hiyo ni heshima kwa Jimbo letu na kwa Kanisa Katoliki Tanzania, na hivyo tunaomba Mwenyezi Mungu azidi kuwaongoza na kuwajalia neema na hekima katika kutuongoza sisi raia na wananchi wenu.”

Naye Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania anayemaliza muda wake, Mhashamu Askofu Mkuu Angelo Accattino, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki, akisema ushiriki wa viongozi wa Serikali na viongozi wa dini mbalimbali katika maadhimisho hayo ni ishara ya mahusiano mema kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Mpanda mwaka 2001, huku viongozi wa Kanisa wakieleza kuwa katika kipindi hicho Jimbo limepiga hatua katika huduma za kichungaji, elimu, afya na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya jamii.

Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa Kanisa, waamini na wananchi wa Jimbo Katoliki la Mpanda kwa kufanikisha Jubilee hiyo, akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga jamii yenye amani, mshikamano na maendeleo.


























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...