Na Janeth Raphael - MichuziTv

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesema litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo bora, ufugaji wa kisasa na uvuvi wa kitaalamu hata baada ya kuhitimishwa kwa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, alipokuwa akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoshiriki maonesho hayo.

Amesema ushiriki wa JKT, kupitia taasisi zake ikiwemo SUMA JKT, unalenga kuwajengea wananchi uelewa wa mbinu bora za uzalishaji katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, pamoja na kuwaonesha fursa mbalimbali zinazoweza kuwainua kiuchumi.

Meja Jenerali Mabele amesema utoaji wa elimu hiyo hautakoma mara baada ya maonesho kufungwa, bali utaendelea katika eneo hilo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maarifa yanayowawezesha kuongeza uzalishaji na tija.

"Maonesho haya ya Nane Nane kwetu ni endelevu. Hata baada ya maonesho kufungwa, tutaendelea kuwepo hapa kwa lengo moja kubwa la kuendelea kuelimisha Watanzania namna ya kufanya kilimo bora, ufugaji bora na kuendesha shughuli za uvuvi kwa utaalamu zaidi," amesema Meja Jenerali Mabele.

Ameeleza kuwa elimu hiyo inatolewa na wataalamu kutoka JKT, wakiwemo maafisa, askari, vijana wanaohudumu katika jeshi hilo pamoja na watumishi wengine wa umma wenye utaalamu katika sekta hizo.

Kwa mujibu wake, wananchi wanaotembelea banda la JKT wanapata nafasi ya kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji, kuona bidhaa zinazozalishwa na vijana wa JKT pamoja na kufahamu shughuli wanazotekeleza wakati wa mafunzo yao.

Aidha, amesema JKT inashiriki Maonesho ya Nane Nane katika kanda mbalimbali nchini zikiwemo Arusha, Morogoro, Lindi, Mbeya na Simiyu, ambapo wananchi wanaendelea kunufaika na elimu kuhusu kilimo, ufugaji na uvuvi.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Meja Jenerali Mabele amesema JKT inaendelea kusisitiza matumizi bora ya ardhi kwa kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija hata katika maeneo madogo, hatua inayoweza kuongeza kipato na kuimarisha usalama wa chakula.

Amewahimiza wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kutembelea mabanda ya JKT katika viwanja vya Nzuguni ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana wa JKT na kupata elimu itakayowasaidia kuboresha shughuli zao za uzalishaji.

"Niwakaribishe sana Watanzania wote. Wanapofika katika viwanja vya Nane Nane hapa Nzuguni, wasikose kutembelea mabanda ya Jeshi la Kujenga Taifa ili wajionee kazi zinazofanywa na vijana wetu na kupata elimu mbalimbali itakayowasaidia kujiletea maendeleo," amesema.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...