Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ameiagiza Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kuongeza elimu kwa umma kuhusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia, ili Watanzania waelewe manufaa yake na matumizi chanya katika maisha na maendeleo ya taifa.
Prof. Nombo ametoa agizo hilo Agosti 20, 2026 jijini Tanga alipotembelea banda la TAEC katika Maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara kuanzia Agosti 15 hadi 24.
Amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuondoa hofu na dhana potofu kuhusu teknolojia ya nyuklia, huku akisisitiza umuhimu wa kuwajengea wananchi uelewa kuhusu matumizi yake katika sekta mbalimbali.
Prof. Nombo amewataka wataalamu wa TAEC kuendelea kujenga uwezo wa wataalamu wengine wa ndani, ili Tanzania iwe na rasilimali watu wenye ujuzi wa kutosha wa kutumia na kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa manufaa ya taifa.
Ameeleza kuwa serikali imeendelea kutoa fursa za masomo na ufadhili (scholarship) kwa Watanzania wanaosomea fani zinazohusiana na teknolojia ya nyuklia, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na kujenga uwezo wa nchi katika eneo hilo.
Aidha, Prof. Nombo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kushiriki katika mkutano wa kimataifa unaohusisha masuala ya teknolojia ya nyuklia ambayo ni ishara ya umuhimu na fursa ya Tanzania kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine katika sekta hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea maelekezo hayo, Mtafiti Mwandamizi kutoka TAEC, Eng. Christina Paul Nyakyi, amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi kwa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Amesema TAEC itaendelea kuweka mkazo katika matumizi ya teknolojia hiyo kwa maendeleo ya taifa, pamoja na kuwaandaa wataalamu wa ndani watakaoweza kushiriki katika matumizi na uendelezaji wa teknolojia ya nyuklia nchini.


.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...