Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Kijiji cha Ushirika kilichoandaliwa katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa jijini Dodoma kimeonesha kwa vitendo mchango mkubwa wa ushirika katika kukuza uchumi wa wakulima kupitia uzalishaji, masoko, huduma za kifedha na uongezaji thamani wa mazao.
Akizungumza katika Siku ya Ushirika iliyofanyika ndani ya Kijiji cha Ushirika kwenye maonesho hayo Agosti 8, 2026, amesema kijiji hicho si eneo la maonesho pekee, bali ni sehemu ya kuonesha namna ushirika unavyoendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuwahudumia wakulima na wanaushirika katika nyanja mbalimbali.
Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amepongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) kwa kusaini mkataba wa makubaliano ya kiutendaji, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kumkwamua mkulima kwa kumpatia huduma ya bima ya uhakika itakayomwezesha kutekeleza shughuli zake bila vikwazo.
Naye Mrajis Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini, Benson Ndiege, amesema Kijiji cha Ushirika kimeandaliwa ili kuonesha namna mfumo wa ushirika kupitia vyama vyake unavyoweza kuwahudumia wanaushirika kuanzia uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao, pamoja na huduma za kifedha kupitia vyama vya akiba na mikopo na huduma za bima.
Amesema kupitia maonesho hayo, vyama vya ushirika vimepata nafasi ya kuonesha kwa vitendo ubunifu na mchango wake katika kuinua maisha ya wakulima, huku vikionesha huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa kwa wanachama wake katika mnyororo mzima wa thamani.



.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...