Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema maandalizi ya Kongamano la 5 la Kimataifa la Uchumi wa Buluu yanaendelea vizuri. Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, huku washiriki kutoka zaidi ya nchi saba wakitarajiwa kuhudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 20 Agosti 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa DMI, Prof. Gurumo amesema kongamano hilo limeandaliwa na DMI, chini ya Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, likiwa na kaulimbiu “Kuwezesha Shughuli za Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika.” Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

Prof. Gurumo amesema kongamano hilo linafanyika wakati Tanzania ikiendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku utajiri wa Bahari ya Hindi, maziwa, mito, visiwa na rasilimali nyingine za maji yakiwa na fursa kubwa katika kuchochea uwekezaji, biashara, ajira, usalama wa chakula, usafiri, utalii, nishati, utafiti na teknolojia.

Ameeleza kuwa kongamano litakuwa jukwaa la kuunganisha tafiti, maarifa, sera, teknolojia na wadau mbalimbali katika kujadili fursa, changamoto na suluhisho za matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu kwa maendeleo endelevu. Msisitizo utawekwa katika utafiti na ushahidi wa kisayansi, uwekezaji, ushiriki wa sekta binafsi na wananchi, ubunifu na kujenga uwezo wa kitaasisi, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024.

Katika kongamano hilo, wataalamu, watafiti na wanazuoni wanatarajiwa kuwasilisha tafiti na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali, yakiwemo bandari na usafiri wa majini, mazingira ya bahari, mabadiliko ya tabianchi, uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini, sheria za bahari, teknolojia, ujasiriamali, elimu na mafunzo ya bahari, usalama wa bahari na uwekezaji.

Prof. Gurumo amesema kongamano linatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali, yakiwemo China, Afrika Kusini, Sweden, Japan, Canada, Russia, Thailand, Morocco, Kenya, Comoro na Uturuki, kwa ajili ya kubadilishana maarifa, teknolojia na uzoefu, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukabiliana na changamoto za bahari.

Kwa upande wa DMI, Prof. Gurumo amesema kongamano hilo ni sehemu ya jukumu la Chuo la kuwa kitovu cha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya bahari na Uchumi wa Buluu. Kongamano linatarajiwa kutoa maarifa mapya, mapendekezo ya kisera yanayotokana na ushahidi wa kisayansi, fursa za utafiti na ushirikiano wa kitaaluma na kitaasisi, pamoja na fursa za ubunifu na uwekezaji.

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amewakaribisha wataalamu, watafiti, wanazuoni, wawakilishi wa sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za kitaifa na kimataifa, wadau wa maendeleo pamoja na jumuiya ya kitaaluma kushiriki katika Kongamano la 5 la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, linaloandaliwa na DMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Uchukuzi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...