Na George Maziku, Geita
HOSPITALI ya Gakala iliyopo kijiji cha Masumbwe, kata ya Bukandwe, wilaya ya Mbogwe inategemea kupokea jopo la madaktari bingwa watakaotoa huduma mbalimbali kuanzia tarehe 17 Agosti, mwaka huu mpaka tarehe 21.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo Bunga Dadu Gakala wakati alipozungumza na jopo la waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake.
Alisema kuwa lengo la kuendesha kambi hiyo ni kuwapunguzia wananchi wa wilaya ya Mbogwe na wilaya zingine jirani, gharama za kufuata huduma za matibabu zinazotolewa na madaktari bingwa.
“Hospitali ya Gakala inawatangazia wakazi wa Masumbwe kuwa kutakuwa na madaktari bingwa kuanzia Jumatatu tarehe 17 mpaka 21, mwezi huu. Tutapokea madaktari bingwa 5 wa magonjwa ya kina mama, daktari bingwa wa watoto, daktari bingwa wa upasuaji, daktarin bingwa wa mifupa na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kama vile sukari, presha na magonjwa mengine yote ya ndani.
“Kwahiyo tunawakaribisha sana wananchi wote wa Masumbwe na maeneo mengine mbalimbali ya wilaya ya Mbogwe na hata wilaya za jirani, waje wapate huduma za mabingwa wa tiba”, alisema Gakala.
Amezitaja huduma zitakazotolewa na madaktari hao kwa kina mama kuwa ni afya ya uzazi, ushauri na vipimo kabla ya ujauzito, matatizo ya kutopata mtoto (Ugumba), uangalizi kipindi cha ujauzito, Ultrasound kwa wajawazito na wasio wajawazito na kutokwa uchafu au damu isiyo kawaida sehemu za siri.
“Pia madaktari hao watatoa matibabu ya uvimbe katika nyonga au tumbo, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matatizo yatokanayo na hedhi na ukomo wa hedhi”, alifafanua Gakala.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa imekuwa kawaida kwa hospitali yake kupokea madaktari bingwa kwa lengo la kuwapatia wananchi wa Masumbwe fursa ya kupata huduma za matibabu karibu na makazi yao badala ya kusafiri mbali kutafuta huduma hizo.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...