Na Avila Kakingo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Afrika inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu na uwekezaji ili kufikia malengo ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na matokeo yake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika, Dk. Samia amesema bara hilo limekuwa na maono na mipango mbalimbali ya maendeleo kwa muda mrefu, lakini sasa kinachohitajika ni utekelezaji wa miradi yenye matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Amesema wananchi hawapimi maendeleo kwa ahadi au matamko, bali kwa uwepo wa miundombinu bora kama barabara, reli, bandari, nishati ya uhakika na mifumo ya kidijitali inayochochea biashara, kuvutia uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii.

"Ni wakati wa kugeuza mawazo kuwa miradi, ushirikiano kuwa uwekezaji na fursa za Afrika kuwa ustawi wa watu wetu," amesema.

Amesema dunia inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, misukosuko ya uchumi wa dunia na upungufu wa mitaji, hali inayolazimu Afrika kujitegemea zaidi kwa kuwekeza katika rasilimali zake na kuongeza biashara ndani ya bara kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Amesema Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ikiwemo upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), viwanja vya ndege pamoja na miradi ya barabara na nishati ili kuimarisha nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari kama Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kuhusu sekta ya nishati, amesema Tanzania imeongeza uzalishaji wa umeme kupitia maji, gesi asilia na vyanzo vingine vya nishati safi ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi.

"Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya kidijitali ili kuongeza ubunifu, huduma za kifedha na fursa kwa vijana na wajasiriamali," amesema.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema Serikali inalenga kujenga uchumi wa kisasa unaoshindana kimataifa, huku sekta binafsi ikitarajiwa kutekeleza zaidi ya asilimia 70 ya uwekezaji unaohitajika katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Amewahimiza wawekezaji na taasisi za kifedha kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo usafirishaji, nishati, viwanda, usafirishaji wa mizigo na uchakataji wa bidhaa ili kuongeza thamani ya rasilimali za Afrika.

Aidha, ameipongeza Africa50 kwa mchango wake katika kufadhili na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu barani Afrika, akisema taasisi hiyo ni mfano wa namna Waafrika wanavyoweza kushirikiana kujenga mustakabali wa bara lao.

Katika mkutano huo, hati mbalimbali za makubaliano zilisainiwa zikiwemo za ushirikiano katika huduma za matibabu ya figo, miradi ya usambazaji wa umeme pamoja na mpango wa usafirishaji wa gesi asilia kwenda katika nchi nyingine za Afrika.

Kwa upande wake, Naibu wa Rais wa Kenya, Prof. Kithure Kindiki, amesema maendeleo ya viwanda na uchumi yanategemea upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na inayowafikia wananchi kwa urahisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu mikubwa ya uzalishaji na usambazaji wa nishati pamoja na sera zinazovutia uwekezaji.

Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kaulimbiu ya mkutano huo ya "Kutoka Maono hadi Matokeo" inalenga kuhimiza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha miradi mikubwa inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayoonekana.

Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mwenyekiti wa Bodi ya Africa50, Dk. Sidi Ould Tah, amesema maadhimisho ya miaka 10 ya taasisi hiyo yanaashiria mafanikio makubwa katika kuhamasisha uwekezaji wa miundombinu barani Afrika, huku akisisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuharakisha utekelezaji wa miradi badala ya kubaki kwenye maono pekee.






Matukio mbalimbali katika picha 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...