Na Janeth Raphael - MichuziTv

Serikali imesema Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ‘Nanenane’ yamefungua fursa mpya za masoko ya nje kwa wakulima wa Tanzania, baada ya baadhi ya mazao ya kilimo kuanza kupata nafasi ya kuuzwa moja kwa moja katika soko la Sudan Kusini.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kuongezeka kwa ushiriki wa wadau wa ndani na nje ya nchi katika Maonesho ya Nanenane, ambayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi kutoka masoko mbalimbali.

“Maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wakulima na masoko. Ushiriki wa nchi mbalimbali umeleta manufaa makubwa na tayari mazao yetu yataweza kuuzwa moja kwa moja katika soko la Sudan Kusini,” alisema Chongolo.

Ameema Serikali imekuwa ikisisitiza maonesho hayo kufanyika kwa mtazamo wa kimataifa ili yaweze kuwasaidia wazalishaji wa Tanzania kupata masoko mapya, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na hatimaye kuongeza kipato cha wakulima.

Kwa mujibu wa Chongolo, jumla ya washiriki 1,668 kutoka ndani na nje ya nchi walishiriki katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, huku nchi zilizoshiriki zikijumuisha China, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Urusi, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi, Israel na Marekani.

Amesema pia wakulima, wavuvi na wadau wengine 286 waliokuwa waoneshaji walipata fursa ya kuonyesha bidhaa, ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Chongolo amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma za ugani kwa wakulima kupitia Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani, unaoshirikiana na sekretarieti za mikoa hadi ngazi ya vijiji ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu na ushauri wa kitaalamu unaohitajika kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.

Katika kuwawezesha vijana kushiriki zaidi katika kilimo, alisema mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) umeendelea kutoa fursa kwa vijana kuingia katika shughuli za uzalishaji, ambapo ekari 126,180 zimeandaliwa katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumzia uzalishaji wa mazao ya mafuta, Chongolo alisema Serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Alisema Tanzania kwa sasa huzalisha takribani tani 300,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ya ndani yanafikia tani 700,000, hivyo nchi hulazimika kuagiza nje takribani tani 400,000 kwa mwaka.

Amesema hali hiyo inaifanya Tanzania kutumia zaidi ya dola milioni 200 kwa mwaka kuagiza mafuta kutoka nje, jambo lililosababisha Serikali kuweka mkakati maalumu wa kuongeza uzalishaji wa ndani na kuongeza kipato kwa wakulima.

Kwa kuanzia, Serikali imetambua Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu katika utekelezaji wa mkakati huo. Chongolo alisema hatua hiyo itaenda sambamba na ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao ili kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuwawezesha wakulima kupata thamani zaidi ya mazao yao.

Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za fedha kuwawezesha vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo kupata mikopo pamoja na elimu ya kilimo na biashara kupitia mpango wa BBT.

Chongolo amesema Shilingi bilioni 300 zitatolewa kupitia benki mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo kupata mikopo. Benki hizo ni pamoja na CRDB, Stanbic Bank, NBC, TCB, Azania Bank, Benki ya Ushirika na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ambayo ni mdhamini mkuu wa Maonesho ya Nanenane.

Kuhusu uendelezaji wa Maonesho ya Nanenane, Chongolo alisema Serikali inapendekeza maonesho hayo yaendelee kufanyika katika viwanja hivyo kutokana na uwezo wake wa kuhudumia washiriki na wananchi wengi, huku uzinduzi wake ukifanyika kwa kuzunguka katika kanda mbalimbali nchini.

Amesema utaratibu huo utasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa fursa ya kushiriki katika maonesho hayo, huku wakulima na wadau wengine wakipata nafasi pana zaidi ya kuonyesha bidhaa zao, kutafuta masoko na kuunganika na fursa za biashara ndani na nje ya nchi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...