Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umeeleza kuwa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja umeendelea kuhakikisha Tanzania inapata bidhaa za mafuta kwa uhakika, kwa wakati na kwa gharama shindani.

Akizungumza katika Maonesho ya Nne ya Kitaifa ya Utamaduni yanayoendelea mkoani Morogoro, Mchumi wa PBPA, Bw. Henry Kilenga, amesema mfumo huo unahusisha ukusanyaji wa mahitaji ya mafuta kutoka kwa kampuni za uuzaji wa mafuta nchini kabla ya kutangazwa kwa zabuni za kimataifa.

Amesema PBPA hukusanya mahitaji hayo na kuyaunganisha ili mafuta yaagizwe kwa pamoja kwa kiwango kikubwa. Utaratibu huo huiwezesha nchi kunufaika na ununuzi wa pamoja na kupata gharama shindani za uagizaji na usafirishaji.

“PBPA hukusanya mahitaji ya mafuta kutoka kwa kampuni za uuzaji wa mafuta, huandaa zabuni na kuwashindanisha wazabuni waliokidhi vigezo. Utaratibu huu unasaidia kuhakikisha nchi inapata mafuta kwa uhakika na kwa gharama shindani,” amesema Kilenga.

Amefafanua kuwa zabuni hizo hushirikisha kampuni za kimataifa zilizohakikiwa na kukidhi vigezo vilivyowekwa na PBPA. Wazabuni hushindanishwa kwa uwazi, huku tathmini ikizingatia bei zilizowasilishwa, uwezo wa kusambaza mafuta na masharti mengine ya zabuni.

Kwa mujibu wa Kilenga, baada ya kukamilika kwa tathmini, kampuni zilizokidhi vigezo na kuwasilisha bei nzuri huchaguliwa kuleta mafuta nchini kulingana na kiasi na muda uliopangwa.

Kilenga amesema uwazi na ushindani katika uendeshaji wa zabuni unalenga kulinda maslahi ya taifa, kuongeza ufanisi na kuhakikisha bidhaa za mafuta zinaendelea kupatikana kwa ajili ya wananchi na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Amesisitiza kuwa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja una mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...