Wakulima katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameendelea kunufaika na huduma za malipo ya kidijitali zinazotolewa na Mixx by Yas, zinazowawezesha kupokea fedha za mazao moja kwa moja kupitia simu zao na kupunguza ulazima wa kusafiri umbali mrefu kufuatilia malipo.

Huduma hizo zimekuwa na umuhimu zaidi kwa wakulima waliopo maeneo ya vijijini na mbali na taasisi za kifedha, kwa kuwapa njia rahisi na salama ya kupokea na kufuatilia fedha zao baada ya kuuza mazao.

Akizungumza wakati wa kilele cha Maonesho ya Kilimo ya Nanenane katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Meneja wa Biashara wa Mixx by Yas Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Charles Gardner, alisema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yanaendelea kuondoa baadhi ya changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo katika kupokea fedha za mazao.

Gardner alisema kupitia Mixx, mkulima anaweza kupokea malipo moja kwa moja kwenye simu yake bila kulazimika kusafiri kwenda kufuata fedha, hali inayookoa muda na gharama huku ikipunguza utegemezi wa fedha taslimu.

“Tunataka mkulima aweze kupokea fedha za mazao yake kwa urahisi popote alipo. Badala ya kutumia muda na gharama kusafiri kufuatilia malipo, fedha zinaweza kumfikia moja kwa moja kupitia simu yake na akazitumia kulingana na mahitaji yake,” alisema Gardner.

Alisema Mixx by Yas inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali na namna zinavyoweza kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Baadhi ya wakulima wanaotumia huduma hizo wamesema malipo kupitia simu yamepunguza muda waliokuwa wakitumia kusubiri au kufuatilia fedha baada ya kuuza mazao yao.

Joyce Mube, mkulima kutoka Tunduma, alisema mfumo huo umemrahisishia kupokea na kufuatilia malipo ya mazao yake bila kulazimika kusafiri kwenda kufuata fedha.

“Unapopokea fedha kupitia simu unakuwa na uhakika wa malipo yako na unaweza kuyafuatilia kwa urahisi. Pia inapunguza muda na gharama ambazo tungetumia kwenda kufuata fedha,” alisema Mube.

Wakati huohuo, Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Roodny Alananga, amewataka wakulima na wajasiriamali kuzingatia ubora na viwango vya bidhaa zao ili kuongeza ushindani na kupata fursa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alananga alisema elimu inayotolewa na TBS inalenga kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kuboresha bidhaa zao na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko mbalimbali.

Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wakulima kukutana na wadau wa sekta ya kilimo na kupata taarifa kuhusu teknolojia, huduma za kifedha, masoko na viwango vya bidhaa zinazoweza kusaidia kuongeza tija na kipato.
Meneja wa Biashara wa Mixx - Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Charles Gardner

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...