SAME.
SERIKALI ya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kumuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina limehifadhiwa, ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Jiungeni, iliyopo Kata ya Ruvu wilayani humo baada ya kubainika kuwa familia yake ilimkatisha masomo na kumpeleka kwa mwanaume kwa lengo la kumuozesha.
Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema Serikali ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu mtoto huyo kuozeshwa, ambapo alituma maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi na walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 kama Mume na Mke.
“Serikali inalaani vikali kitendo hiki cha kikatili cha kumnyima mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu na kukua katika mazingira salama, mpaka sasa watuhumiwa tayari wapo mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria na niwaombe wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kuhusu vitendo vya aina hiyo" Alisema Kasilda.
Aidha, Kasilda alisema shule ya Jiungeni ilijengwa mahususi kwa ajili ya kuwakomboa watoto wa jamii ya Kifugaji wanaoishi katika eneo hilo huku akieleza huenda kuna wanafunzi wengine walioacha shule kutokana na ndoa za utotoni au kwenda kuchunga mifugo.
Alisisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu. Amesema.
“Msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni lazima watoto waende shule na sisi tutapambana na wazazi wanaokiuka maelekezo ya Serikali.” alisema.
Aliwapongeza maafisa wa Serikali na wananchi waliofanikisha zoezi hilo na kumwokoa mtoto huyo kwa kushirikiana na wananchi wema, wakifanya uchunguzi katika mazingira magumu ya porini ambako mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana huyo kama mke.
Kasilda pia amewaonya baadhi ya watu wanaopanga kutoa rushwa kwa lengo la kuwaachia watuhumiwa akieleza kuwa watakaobainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehatarisha usalama, elimu na ustawi wa watoto na kusisitiza kuwa mtoto huyo atarejeshwa shuleni.
Ndoa za utotoni zina madhara makubwa kwa watoto, ikiwemo kuwanyima fursa ya elimu na kuwaweka katika hatari ya ukatili, unyanyasaji pamoja na changamoto za kiafya na kisaikolojia.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa watoto kulindwa, kupata elimu na kukua katika mazingira salama yanayozingatia maslahi na mustakabali wao.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...