Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kuimarisha sekta za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi kwa kuongeza thamani ya bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, wakati akizungumza katika mjadala kuhusu Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na kufanyika katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma.

Mjadala huo uliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi na taasisi zinazohusika na maendeleo ya sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Londo alisema Serikali imekuwa ikiratibu shughuli mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alisema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na kilimo, ufugaji na uvuvi, kwa lengo la kupata taarifa na teknolojia zitakazosaidia kuongeza tija na ubora wa bidhaa.

“Serikali inaendelea kuratibu shughuli mbalimbali, ikiwemo kufanya tafiti katika maeneo ya kilimo, ufugaji na uvuvi, kwa lengo la kuongeza uzalishaji unaoendana na kuongeza thamani ya bidhaa ili ziweze kupata masoko ndani na nje ya nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi ni hatua muhimu katika kuwawezesha wazalishaji kupata kipato zaidi, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

FAO YAWEKA MKAZO MNYORORO WA THAMANI
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania, Dkt.Nyabenyi Tipo, katika mijadala na wadau mbalimbali kuhusu uimarishaji wa mnyororo wa thamani wa kilimo chenye tija.

Alisema mjadala huo unalenga kuongeza tija katika kilimo, kupunguza upotevu wa mazao na kuhakikisha wakulima wanaongeza kipato kutokana na shughuli zao.

Tipo alisema FAO inalenga kuhakikisha mnyororo mzima wa uzalishaji, kuanzia shambani hadi sokoni, unaimarishwa ili mkulima,Mfugaji na pamoja Mvuvi waweze kunufaika zaidi na shughuli za kilimo.

Alisema katika kuimarisha mnyororo huo, ni muhimu kuweka mikakati ya kupunguza upotevu wa mazao unaotokea baada ya kuvuna, hususan katika hatua za usindikaji, uhifadhi na usafirishaji.

Aidha, alisema ni muhimu kuwaunganisha wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wasindikaji, taasisi za fedha, watafiti na Serikali, ili kujenga mfumo unaowezesha kila mdau kunufaika na mnyororo wa thamani.

Tipo pia alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia na data katika kuendeleza kilimo cha kisasa kinachozingatia mahitaji ya soko pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.

Alisema matumizi ya teknolojia yanaweza kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi kuhusu masoko, uzalishaji na hali ya hewa, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zinazowakabili katika uzalishaji.

Alisema FAO Tanzania imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Kilimo, taasisi za utafiti, mashirika ya kiraia na sekta binafsi katika kujadili na kubuni mikakati ya kuimarisha mifumo ya chakula nchini.

Alisema ushirikiano huo unalenga kujenga mnyororo wa thamani wa kilimo ulio imara na wenye tija, ambao utaongeza thamani ya mazao, kuboresha kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...