Akihitimisha Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi bilioni 300 kwa wakurugenzi wa taasisi hizo saba za kifedha, akisisitiza umuhimu wa kuongeza fursa za kifedha kwa makundi hayo ya kijamii ili yaweze kushiriki kikamilifu na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na sekta ya kilimo.
Akizungumzia utayari wa benki hiyo kutekeleza mpango huo, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa NBC, Bw. Jacob Nangi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini NBC katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya uwezeshaji, hususan inayolenga vijana, wanawake na sekta ya kilimo.
Alisema NBC tayari imejipanga kutekeleza dhamira hiyo kwa kuendelea kubuni bidhaa na suluhisho za kifedha zinazokwenda sambamba na mahitaji ya makundi hayo.
“Pamoja na kuipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa hatua hiyo na kuona NBC inastahili kuwa mmoja wa wadau muhimu katika kufanikisha mpango huu, nisisitize utayari wetu wa kufanikisha mpango huu kulingana na malengo ya Serikali ya kuwasaidia vijana na wanawake nchini kushiriki na kunufaika kikamilifu na fursa mbalimbali zinazotokana na mnyororo mzima wa sekta ya kilimo,” alisema Bw. Nangi.
Akieleza hatua zinazochukuliwa na NBC kuthibitisha dhamira yake ya kuiwezesha sekta ya kilimo, Bw. Nangi alisema benki hiyo imeendelea kwenda hatua moja zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida za kibenki kwa wakulima, kwa kubuni suluhisho zinazolenga changamoto na mahitaji mbalimbali yanayojitokeza katika mnyororo mzima wa thamani.
Katika kilele cha Maonesho hayo, NBC ilikabidhi rasmi malori 13 kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya RUNALI na Lindi Mwambao vya mkoani Lindi, na hivyo kufanya idadi ya malori yaliyotolewa na benki hiyo kwa vyama vya ushirika kufikia 28, baada ya kukabidhi malori mengine 15 kwa vyama vya TANECU na KACU mapema wiki iliyopita. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa vyama hivyo kusafirisha mazao ya wakulima kwa ufanisi zaidi.
Benki hiyo pia ilikabidhi mkopo wa uboreshaji wa makazi kwa Bw. Emmanuel Nyambi Masanja, mkulima na mwanachama wa AMCOS ya Kasandalala, iliyopo Ushetu wilayani Kahama. Bw. Masanja ni miongoni mwa wakulima 57 waliowezeshwa na NBC kupitia mpango wa mikopo ya uboreshaji wa makazi kwa wakulima.
“Jitihada zote hizi zinaakisi mkakati wa NBC wa kwenda hatua moja zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida za kibenki kwa wakulima. Tunataka kutoa suluhisho zinazogusa mahitaji muhimu katika mnyororo mzima wa thamani—kuanzia uzalishaji, upatikanaji wa mitaji, usafirishaji na uhifadhi wa mazao hadi kuboresha maisha na makazi ya wakulima,” aliongeza Bw. Nangi.
Akifafanua kuhusu uwezeshaji huo, Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa, alisema kati ya malori 13 yaliyokabidhiwa kwenye kilele hicho, 10 yamekwenda kwa RUNALI na matatu kwa Lindi Mwambao.
Alisema uwezeshaji huo unalenga kuongeza uwezo wa vyama hivyo kusafirisha mazao kwa ufanisi, kupunguza changamoto za usafirishaji na hatimaye kuongeza thamani inayobaki kwa wakulima.
“Tofauti na mkopo wa malori 15 mengine tuliyokabidhi kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) hivi karibuni, mkopo huu kwa RUNALI na Lindi Mwambao una thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.5, na unatarajiwa kuboresha ufanisi wa shughuli za ushirika na kuongeza uwezo wa wakulima kufikisha mazao yao kwenye masoko,” alisema Bw. Urassa.
Hafla ya makabidhiano hayo ilishuhudiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ambaye alisema uwezeshaji huo unaendana na msisitizo wa Serikali wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za fedha na vyama vya ushirika kama njia muhimu ya kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Dkt. Ndiege alisema ushirika una nafasi muhimu katika kuwaunganisha wakulima na taasisi rasmi za kifedha, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi na kupata huduma zinazokidhi mahitaji yao.
“Hatua hii inaonyesha upanuzi wa mtazamo wa huduma za kifedha kwa wakulima, ambapo mkulima haonekani tu kama mzalishaji wa mazao, bali pia kama mteja mwenye mahitaji ya kifedha yanayogusa ustawi wa familia yake na maisha yake kwa ujumla,” alisema.
Alisema ameguswa pia na mpango wa NBC wa mikopo ya uboreshaji wa makazi ya wakulima, akieleza kuwa mpango huo unaweza kusaidia kubadilisha mtazamo wa muda mrefu wa kutolipa kipaumbele suala la makazi bora kwa wakulima.
“Zaidi, kupitia mpango huu wa mikopo ya uboreshaji wa makazi, wakulima wengi watashawishika kuingia kwenye ushirika ili wanufaike na fursa hii. Pia watahakikishiwa maboresho ya makazi yao kwa sababu huduma inatangulia, kisha malipo yanafanyika baada ya mkulima kuuza mazao yake. Nawashukuru na kuwapongeza sana NBC kwa kubuni mpango huu,” alisema Dkt. Ndiege.
Kwa upande wao, viongozi wa vyama vya ushirika vilivyonufaika na uwezeshaji huo pamoja na mkulima aliyepokea mkopo wa uboreshaji wa makazi waliipongeza NBC kwa kuendelea kubuni bidhaa zinazolenga mahitaji halisi ya wakulima.
Mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Bw. Ismail Nalinga, Mwenyekiti wa RUNALI, Bw. Odas Odas Mpunga, na mkulima Emmanuel Nyambi Masanja, walisema mfumo wa mauzo ya mazao kupitia vyama vya ushirika umeendelea kuimarika na hivyo kuvifanya vyama hivyo kuwa daraja muhimu kati ya wakulima na taasisi rasmi za fedha.
Bw. Mpunga alisema maboresho katika mfumo wa mauzo ya mazao kupitia vyama vya ushirika yameongeza uaminifu na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima.
“Mfumo wa mauzo ya mazao kupitia vyama hivi vya ushirika umeziwezesha benki kama NBC kuwa na msingi unaotuwezesha kunufaika na huduma zao, hususani mikopo, kwa usahihi zaidi. Kwa msingi huo, sisi kama wakulima kwa sasa tumekaribiwa na taasisi za fedha kuliko wakati mwingine wowote,” alisema.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (kushoto) akikabidhi picha ya inayosadifu muonekano wa nyumba iliyofanyiwa maboresho kwa Bw. Emmanuel Nyambi Masanja (kulia), mkulima na mwanachama wa AMCOS ya Kasandalala, iliyopo Ushetu wilayani Kahama ambae ni miongoni mwa wakulima 57 waliowezeshwa na NBC kupitia mpango wa mikopo ya uboreshaji wa makazi kwa wakulima. Tukio hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki kwenye Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege pamoja na maofisa wengine wa benki ya NBC.
Akihitimisha Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) alikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi bilioni 300 kwa wakurugenzi wa taasisi saba za kifedha ikiwemo NBC akilenga kuongeza fursa za kifedha kwa wanawake na vijana waweze kushiriki kikamilifu na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na sekta ya kilimo.
Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa (wa pili kulia) akifafanua kuhusu huduma mbalimbali za benki hiyo mahususi kwa wakulima mbele Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege pamoja na wadau wengine.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa ufunguo wa gari Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Lindi Mwambao, Bw. Ismail Nalinga (wa pili), ikiwa ni ishara ya makabidhiano rasmi ya malori matatu (3) yaliyowezeshwa kupitia mkopo wenye riba nafuu kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Malori hayo yanalenga kuboresha usafirishaji wa mazao, kuongeza ufanisi wa shughuli za ushirika na kuimarisha kipato cha wakulima. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa (kulia) na Meneja wa Benki ya NBC tawi la Dodoma Bi Happyness Kizigira (kushoto)
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (katikati) akionyesha cheti cha kutambua ushiriki na udhamini wa benki hiyo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wengine wanaoonesha ishara ya ‘Tunakuona mbali’ ni maofisa waandamizi wa benki hiyo.
Tunakuona mbali mkulima
Viongozi mbalimbali wa serikali waliapata wasaa wa kutembelea banda la NBC lilikuwepo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane2026 yaliyohitimishwa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...