Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Profesa Tumaini Gurumo akiwa ametembelea Banda la DIT Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu ,Tanga.

Na Mwandishi Wetu, Tanga
MKUU wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini S. Gurumo, amesema hakuna maendeleo ya Taifa yasio na uhusiano na manufaa yatokanayo na sekta ya Bahari.

Katika maendeleo yaliyopo nchini sekta ya Bahari ni kiungo muhimu hivyo wananchi wanatakiwa kuangalia fursa zilizopo sekta hiyo katika maisha ya kila siku

Prof. Gurumo amesema Bahari ina mchango mkubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ikiwamo usafirishaji, biashara, uvuvi na shughuli nyingine zinazochangia maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema kwa msingi huo, kila Mtanzania ni mdau wa sekta ya Bahari kwa namna moja au nyingine, hivyo kuna umuhimu wa jamii kuwa na uelewa mpana kuhusu fursa na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.

Prof. Gurumo aliyasema hayo jijini Tanga katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, alipokuwa akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara,jijini Tanga.

Amesema elimu, ujuzi na ubunifu ni nguzo muhimu katika kuendeleza sekta ya Bahari, kwa kuwa vinawezesha kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kubuni na kutekeleza suluhisho za changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Prof. Gurumo, DMI imeshiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu shughuli zinazofanywa na chuo hicho, pamoja na kuonesha bunifu mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi na wataalamu wake.

Amesema bunifu hizo zinalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii, huku zikitoa fursa kwa vijana kutumia elimu na ujuzi wao kubuni bidhaa na huduma zinazoweza kuchochea maendeleo.

“Ni muhimu jamii kuelewa kwamba sekta ya Bahari inamhusu kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine,” amesema Prof. Gurumo.

Aidha, amewataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kuimarisha sekta hiyo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu, ujuzi na ubunifu ni muhimu kwa Tanzania kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na Uchumi wa Bluu.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza tija, kukuza ajira na biashara, pamoja na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na rasilimali na fursa zinazopatikana kupitia sekta ya Bahari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...