Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetakiwa kuongeza uwekezaji katika tafiti na ubunifu unaofanywa na vyuo vya elimu ya juu nchini ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii na kuongeza mapato ya taifa kupitia teknolojia zinazozalishwa na wataalamu wazawa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Husna Sekiboko, wakati alipotembelea Banda la Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) katika Maonesho ya Wiki ya Elimu Kitaifa, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Tanga.
Sekiboko amesema tafiti na ubunifu unaofanywa na vyuo vya elimu ya juu nchini umefikia hatua kubwa na una uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, hivyo unapaswa kupewa kipaumbele, bajeti na uwezeshaji wa kutosha. Amesema miongoni mwa teknolojia iliyomvutia ni mfumo wa ultrasound uliobuniwa na wataalamu wa UDOM, unaolenga kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa gharama nafuu ikilinganishwa na baadhi ya vifaa vinavyopatikana sokoni. Kwa mujibu wa Sekiboko, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kufuatilia maendeleo ya mtoto akiwa tumboni kuanzia wiki 12 za ujauzito, pamoja na kusaidia katika uchunguzi wa afya ya mama na mtoto.
Amesema ubunifu huo ni mfano wa teknolojia zinazopaswa kuendelezwa na kusambazwa katika vituo vya afya nchini kabla ya Tanzania kuanza kuzisafirisha katika nchi nyingine za Afrika.
“Tunatakiwa kuwekeza na kuendeleza ufumbuzi ambao umefanyika kwa teknolojia hii iweze kukua, lakini isambae na iweze kutumika kwenye vituo vya afya nchi nzima. Baadaye tuuze kwenye nchi za jirani,” amesema.
Amesema Tanzania kwa sasa inatumia teknolojia kutoka nchi mbalimbali, zikiwamo China na India, katika sekta za afya, kilimo na maeneo mengine, hivyo ni wakati muafaka kwa taifa kuanza kuzalisha na kuuza teknolojia zinazobuniwa na wataalamu wa ndani. Sekiboko amesema teknolojia ya ultrasound iliyobuniwa UDOM inaweza kuwa miongoni mwa bidhaa za “Made in Tanzania” zinazoweza kutumika ndani ya nchi na kuuzwa nje, hatua ambayo inaweza kuongeza mapato ya vyuo na taifa, pamoja na kutoa ajira kwa wataalamu watakaohusika katika uzalishaji na matumizi yake.
Amesema ubunifu unaofanywa na vyuo unahitaji bajeti, uwezeshaji na kuunganishwa na masoko ili bidhaa na teknolojia zinazozalishwa ziweze kutumika katika taasisi mbalimbali za Serikali. Ameshauri Serikali kuingia mikataba na vyuo vya ndani kwa ajili ya kupata bidhaa na teknolojia zinazohitajika badala ya kutegemea zaidi bidhaa kutoka nje.
“Serikali ichukue sasa vile ambavyo vinazalishwa kwenye vyuo, iwe ndio outsource yao, badala ya kwenda kununua mashine nyingine au kuingia mikataba na China na kwingineko, waingie mikataba na vyuo,” amesema Sekiboko. Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwezo wa vyuo, kukuza tafiti na kuhakikisha wataalamu waliobuni teknolojia hizo wanapatikana kwa urahisi wakati wa matengenezo au kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
Katika hatua nyingine, Sekiboko ametoa wito kwa wananchi wa Tanga na mikoa jirani, ikiwamo Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Wiki ya Elimu Kitaifa, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika Usagara.
Amesema maonesho hayo ni ya kitaifa na yameshirikisha vyuo na taasisi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya Tanzania, hivyo wananchi wana fursa ya kujifunza kuhusu elimu, ujuzi, tafiti na ubunifu unaofanywa nchini. Amesema wananchi wenye mahitaji ya elimu ya juu, wanaotarajia kuwapeleka watoto wao vyuoni au wanaotaka kujifunza kuhusu fursa za ujuzi na teknolojia wanapaswa kutumia nafasi hiyo kutembelea mabanda yaliyopo katika maonesho hayo.
“Ni jambo la ajabu sana tukifunga haya maonyesho, bado kuna Watanga huko nyumbani hajaja kuji, kushughulikia nini kinaendelea hapa. Wajitokeze, waje watembelee haya mabanda,” amesema.
Amesema ushiriki wa wananchi utasaidia kuongeza uelewa kuhusu kazi zinazofanywa na wasomi, wataalamu na wabunifu nchini, pamoja na namna teknolojia hizo zinavyoweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Amesisitiza kuwa wananchi wote wanapaswa kutumia fursa hiyo kufika Usagara na kujionea ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazoonyeshwa katika maonesho hayo.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...