Farida Mangube Morogoro
Katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji holela wa nyara za Serikali, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha utafiti wa kutumia panya buku wenye uwezo wa kunusa na kubaini nyara hizo katika maeneo mbalimbali ya usafirishaji.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, amesema utafiti huo ni sehemu ya jitihada za chuo hicho za kubuni teknolojia bunifu zitakazosaidia vyombo vya dola kudhibiti biashara haramu ya nyara za Serikali.
Profesa Chibunda alitoa kauli hiyo wakati Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, alipotembelea banda la SUA katika Maonesho ya 88 ya Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro.
Alisema panya hao wamefundishwa kutumia uwezo wao wa kunusa kubaini nyara za Serikali na tayari wameanza kutumika kwa majaribio katika viwanja vya ndege na bandari.
Kwa upande wake, mtafiti kutoka Kituo cha Kudhibiti Wanyama Waharibifu wa Mazao (Pest Management Centre), Princus Mramba, alisema mradi huo ulianza miaka minne iliyopita na kwa sasa umefikia hatua nzuri ya utekelezaji.
Alisema baadhi ya panya hao wamepelekwa nchini Uturuki kushiriki katika shughuli za uokoaji kwa kusaidia kubaini watu waliofukiwa kwenye vifusi baada ya majanga.
Mbali na utafiti huo, Profesa Chibunda alisema SUA pia imeanzisha utafiti wa kutumia bundi kudhibiti panya waharibifu wa mazao mashambani.
Alieleza kuwa, kwa mujibu wa utafiti huo, bundi mmoja ana uwezo wa kula hadi panya 15 kwa siku, hivyo kuwa njia rafiki kwa mazingira katika kupunguza uharibifu wa mazao unaosababishwa na panya.
Aidha, alisema SUA inamiliki Hospitali ya Rufaa ya Wanyama inayotoa huduma za matibabu kwa wanyama wa kufugwa na wanyamapori. Aliongeza kuwa hospitali hiyo pia huwategua wanyama waliokwama kwenye mitego, kuwapatia matibabu na kuwarejesha katika mazingira yao.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...