Na Janeth Raphael – MichuziTv, Dodoma

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, ameeleza kwa kina historia ya mradi wa mafunzo na utafiti wa panya unaoendeshwa na chuo hicho kwa zaidi ya miaka 25, huku akifichua namna panya shujaa Magawa alivyoweka historia duniani kabla ya kufariki.

Prof. Chibunda amezungumza hayo leo jijini Dodoma katika Mkutano na wanahabari, ambapo amesema mradi huo umekuwa ukifanyika SUA kwa zaidi ya miaka 25, ukiwalenga panya wanaofundishwa kufanya kazi mbalimbali za utafiti na huduma za kijamii, huku akibainisha kuwa panya hao wanaotumika katika mradi huo ni wa asili ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, panya hao walitokana na eneo la Milima ya Uluguru mkoani Morogoro, lakini kutokana na kukua kwa mradi huo, SUA kwa sasa ina kituo maalum kinachoshughulikia uzalishaji, malezi na mafunzo ya panya hao.

Amesema mfumo wa malezi na mafunzo ya panya hao umeandaliwa kwa namna ya kipekee chuoni hapo, ambapo kuna maeneo maalum kwa ajili ya panya wanaozalishwa, wanaoanza mafunzo, wanaomaliza mafunzo pamoja na wale wanaostaafu.

“Ukimfika kwetu utakuta tuna wodi ya wazazi, tuna wanaoanza mafunzo, waliohitimu, lakini pia tuna banda la panya wastaafu. Wako pale wanapata pensheni,” amesema Prof. Chibunda.


MAGAWA ALIWEKA HISTORIA CAMBODIA

Akizungumzia panya maarufu duniani Magawa, Prof. Chibunda amesema alikuwa miongoni mwa panya waliopewa mafunzo nchini Tanzania na baadaye kupelekwa Cambodia kwa ajili ya kusaidia kutambua mabomu ya ardhini.

Amesema uamuzi wa kumpeleka Magawa nchini Cambodia ulitokana na ukweli kwamba Tanzania haikuwa na changamoto kubwa ya mabomu ya ardhini kama ilivyokuwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Kusini-Mashariki mwa Asia.

Magawa alifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa na hatimaye kuingia katika historia ya dunia baada ya kugundua idadi kubwa ya mabomu ya ardhini, akivunja rekodi na kuwa miongoni mwa wanyama mashuhuri zaidi waliowahi kutumika katika kazi hiyo.

Uwezo wake wa kugundua mabomu ulimfanya kupata umaarufu mkubwa kimataifa, huku akitunukiwa pia nishani ya heshima kutokana na mchango wake katika kuokoa maisha ya watu na kusaidia kuondoa mabomu hatari yaliyokuwa yamesalia ardhini.


UMRI WA PANYA NA KIFO CHA MAGAWA


Prof. Chibunda amesema panya wanaofundishwa katika mradi huo wana wastani wa maisha wa takribani miaka minane, huku miaka tisa ikiwa ni hatua ya uzee mkubwa kwa panya hao.

Ameeleza kuwa wanapofikia umri huo, huanza kudhoofika kimwili na wanaweza hata kupoteza meno, hali inayowafanya kushindwa kuendelea na shughuli zinazohitaji uwezo mkubwa wa kimwili.

Magawa naye alifikia hatua hiyo ya uzee na hatimaye kufariki dunia akiwa nchini Cambodia, baada ya kutumikia kwa mafanikio katika kazi ya kutambua mabomu ya ardhini.


SUA ILITAKA MAGAWA AREJESHWE TANZANIA

Akijibu swali kuhusu iwapo kulikuwa na mpango wa kumrejesha Magawa nchini Tanzania baada ya kufariki, Prof. Chibunda amesema mpango huo uliwahi kufikiriwa, lakini changamoto za taratibu na vibali vya usafirishaji zilisababisha kutotekelezwa kwa wakati.

“Tunasema ingewezekana, lakini kwa wakati ule taratibu na vibali vya kilojistiki viligoma. Wenzetu kule Cambodia walikosa uvumilivu wa kusubiri, wakamjengea mnara mkubwa kule,” amesema Prof. Chibunda.

Kwa hatua hiyo, Magawa aliendelea kubaki nchini Cambodia ambako alifanya kazi kubwa ya kusaidia kutambua mabomu ya ardhini na kuokoa maisha ya watu.

Historia ya Magawa inaendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya mradi wa SUA wa kufundisha panya kwa matumizi mbalimbali, ikionyesha namna utafiti unaofanywa Tanzania unavyoweza kuzalisha matokeo yenye kutambulika kimataifa.

Mradi huo pia unaendelea kuifanya SUA kuwa miongoni mwa taasisi zinazotumia utafiti na ubunifu katika kutumia uwezo wa wanyama katika kutatua changamoto za kijamii, kiafya na kiusalama.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...