Na Mwandishi Wetu

SERIKALI  imeombwa kuzipa nafasi kampuni zenye uwezo wa kuzalisha gesi ya Okseji ambayo inajukulikana kwa jina la hewa tiba kwa  ajili ya matumizi ya hospitalini kwa kuwa kampuni hizo zinauwezo mkubwa na zimebobea katika uzalishaji huo.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TOL Gases PLC Daniel Warungu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa 31 wa mwaka wa Wanahisa huku akisisitiza wao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha.

Amesema kwa sekta binafsi zinazalisha gesi ya Oksijeni hivyo ni vema Serikali ikawa inanunua badala ya kuzalisha na kupikia mitambo huku akifafanua anaamini serikali itakubali ombi hilo kwa kuwa imeonesha nia huku akisisitiza uwepo wa nyenzo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeonesha jinsi ambavyo sekta binafsi zinavyoweza kuwa mshirika katika utekelezaji wa dira na wao TOL Gases wako tayari.

“Tunafanya uwekezaji mkubwa unaowezesha kuzalisha gesi ya oksijeni kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na hewa tiba kwa ajili ya mahospitalini hivyo ombi letu Serikali badala ya nayo kuwa inazalisha iweke utaratibu wa kuwa inanunua kutoka sekta binafsi.TOL Gases tunao uwezo mkubwa na tumebobea katika uzalishaji wa oksijeni.”

Kuhusu mkutano wa wanahisa Warungu amesema wamejadili masuala mbalimbali huku akieleza kwa upande wa mapato ya kampuni yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 30.2 mwaka 2024 hadi Shilingi bilioni 31.15 mwaka 2025. 

Amefafanua faida kabla ya riba, kodi, uchakavu na punguzo la thamani (EBITDA) iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 10.5 hadi Shilingi bilioni 13.4, huku faida kabla ya kodi ikiongezeka kutoka Shilingi bilioni 3.98 hadi Shilingi bilioni 6.78.”Faida baada ya kodi ilifikia Shilingi bilioni 3.98 mwaka 2025, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 2.06 mwaka 2024.”

Ameongeza TOL Gases inaendelea kuongeza uwezo wake wa uzalishaji kupitia miradi miwili mikubwa. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kiwanda cha Ikama III cha kuzalisha hewa ya ukaa (Carbon Dioxide), kinachotarajiwa kuanza uzalishaji Septemba 2027. Mradi huo utaongeza uwezo wa uzalishaji na kuimarisha upatikanaji wa gesi hiyo.

Aidha kampuni pia inajenga kituo kipya cha kutenganisha hewa (Air Separation Unit – ASU) kwa msaada wa Clinton Health Access Initiative (CHAI). Kituo hicho kinatarajiwa kuanza kufanya kazi Oktoba 2026 na kitaongeza uwezo wa uzalishaji wa oksijeni hadi takribani tani 20 kwa siku, sambamba na kituo kilichoanza kufanya kazi mwaka 2021.

Warungu amesisitiza uwekezaji huo utasaidia kuongeza ufanisi wa uzalishaji, kurahisisha matengenezo ya mitambo bila kuathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji ya gesi katika sekta ya afya, viwanda na uzalishaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni hiyo Leonard Kitoka amesema Tanzania kwa sasa ina uwezo wa kutosha kutoka kwa wazalishaji binafsi kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo ya oksijeni ya tiba, hasa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa hivi karibuni katika mitambo ya uzalishaji.

Akizungumza kuhusu Soko la hisa,amesema  thamani ya hisa za TOL Gases katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka kutoka Shilingi 795 wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliopita hadi kufikia kiwango cha juu cha Shilingi 1,490, sawa na ongezeko la takribani asilimia 74. Kwa sasa, hisa hizo zinauzwa kati ya Shilingi 1,320 na Shilingi 1,490.

“TOL Gases imeeleza kuwa rasilimali za umma zinaweza kutumika kwa ufanisi zaidi katika kuongeza mahitaji na upatikanaji wa oksijeni ya tiba badala ya kuwekeza katika kuongeza zaidi uwezo wa uzalishaji.

“Kampuni inapendekeza hospitali na vituo vya afya kuwezeshwa kununua oksijeni yenye ubora unaohakikishwa kutoka kwa wazalishaji binafsi waliopo, hatua ambayo kwa mujibu wa kampuni itasaidia kutumia kikamilifu uwezo wa uzalishaji uliopo nchini, kuepusha uwekezaji unaojirudia na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa oksijeni kwa gharama nafuu.”

Amesisitiza TOL Gases  itaendelea kushirikiana na Serikali, taasisi za afya na wadau wa maendeleo kuhakikisha upatikanaji wa oksijeni salama na yenye ubora kwa matumizi ya tiba nchini Tanzania, huku ikiendelea kuwekeza katika uzalishaji, usambazaji na utaalamu wa kiufundi.

Pamoja na hayo amesema kutokana na mikakati ya kampuni hiyo wanahisa kwa kauli moja wamekubaliana kutogawana gawio la faida na badala yake fedha hizo za gawio zitumike katika kuwekeza katika Ujenzi wa miundombinu kwanza ili kuongeza mapato ya kampuni.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...