Na Belinda Joseph – Tanga

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetajwa kuwa moja ya taasisi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kutokana na mchango wake katika kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi unaohitajika katika uzalishaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na Michuzi TV Agosti 21, 2026, Meneja Mahusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter, amesema VETA itatumia nguzo tatu kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ambazo ni uchumi imara, jumuishi na shindani, uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, pamoja na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, yanahitaji nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri.

Amesema katika kujenga uchumi imara na shindani, Tanzania inahitaji kuongeza tija katika uzalishaji, kuwekeza katika viwanda na kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi, ambayo yote yanahitaji wataalamu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.

“Tunaposema tufanye uchumi wetu uwe imara na shindani, maana yake tunahitaji kuongeza tija kwenye uzalishaji, tunahitaji uwekezaji kwenye viwanda na tunahitaji utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi, haya yote yanahitaji watu wenye ujuzi na umahiri."

Amesema vijana wanaopata mafunzo kupitia VETA wanaweza kunufaika na fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta za uzalishaji, viwanda na miradi ya maendeleo kupitia ajira na kujiajiri, huku ujuzi ukiwawezesha pia kuongeza ufanisi katika shughuli kama kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji na tija.

Amesema katika kutekeleza nguzo ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, VETA tayari imepanda miti 130,800 katika vyuo vyake kote nchini, huku ikiendelea kutekeleza matumizi ya nishati safi ambapo vyuo 26 tayari vinatumia nishati hiyo, ikiwemo gesi na mkaa mbadala.

Ameongeza kuwa Chuo cha VETA Moshi kwasasa kinazalisha mkaa mbadala unaoweza kutumika kama nishati safi, huku kupitia Mradi wa Elimu na Stadi kwa Ajira zenye tija (ESPJ II) VETA ikipanga kuimarisha programu za usimamizi wa taka, matumizi sahihi ya rasilimali, utunzaji wa mazingira pamoja na afya na usalama mahali pa kazi.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni muhimu katika kujenga nguvu kazi yenye uwezo wa kuchochea tija, ajira na ukuaji wa uchumi, huku hatua za VETA katika mazingira na matumizi ya nishati safi zikiendelea kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...