Wananchi wa Mkoa wa Geita wametakiwa kuendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi Jamii na wananchi, ili kupunguza uhalifu katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Wito huo umetolewa leo Agosti 22, 2026 wakati wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa Polisi Jamii nchini, yaliyofanyika katika Viwanja vya CCM Kalangalala mjini Geita.=
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, amesema ushirikiano baina ya wananchi na polisi umekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha mapambano dhidi ya uhalifu mkoani Geita.
"Ushirikiano huu ndio unaotufanya tuweze kupambana na uhalifu kwa urahisi. Tunaposhirikiana, taarifa zinafika kwa wakati na hivyo tunazuia uhalifu kabla haujafanyika," amesema Shigela.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amezindua rasmi "Polisi Jamii Run Club mpya ya Mkoa wa Geita.
Klabu hiyo itakuwa na jukumu la kuhamasisha wananchi kushiriki mazoezi ya kukimbia mbio nyepesi, huku ikiwa na lengo la kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya askari na jamii.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amekiri kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya wananchi na jeshi la polisi tangu kuanzishwa kwa falsafa ya Polisi Jamii.
Tumekuwa na ushirikiano mkubwa na jeshi la polisi. Leo hii polisi haogopewi tena mtaani kama zamani ambapo alitumika kutishia watoto. Sasa askari na wananchi ni marafiki katika kulinda usalama," amesema Jongo.
Naye Mratibu wa Polisi Jamii Mkoa wa Geita, Amina Kaando, amesema michezo hiyo inalenga kuunganisha jamii na askari ili wananchi waweze kutambua kuwa askari na jamii ni kitu kimoja katika kuzuia na kupambana na uhalifu.
Maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii Mkoa wa Geita yamedhaminiwa na Mgodi wa Dhahabu GGML.
Katika maadhimisho hayo, GGML wamefanikiwa kuwakaribisha washiriki wa Jogging kutoka mikoa mingine ikiwemo Kigoma, Shinyanga na Mwanza.




.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...