Amesema upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi ni muhimu katika kuvutia wawekezaji kwa kuwa mwekezaji anahitaji eneo lililotengwa na kutambuliwa kwa matumizi husika kabla ya kuanzisha shughuli zake.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi katika Kitongoji cha Mwankola, Kata ya Lagangabilili pamoja na kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026 Dkt. Akwilapo amesema hatua hiyo pia inalenga kuzuia migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya makazi, shughuli za kilimo, viwanda na matumizi mengine yanayohitaji maeneo maalumu.
Aidha, Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameeleza kuwa, Wizara yake imejipanga kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maeneo yao yanasimamiwa kwa kuzingatia sheria.
Amewataka wananchi wa Itilima kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazohusu umiliki na matumizi ya ardhi ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha ameeleza kuwa, mkoa wa Simiyu hususan wilaya ya Itilima wanatambua umuhimu wa ardhi hasa katika kumilikisha wananchi, taasisi na vijiji lengo likiwa kuepuka migogoro ya ardhi.
Wakiwasilisha kero yao mbele ya Waziri wa Ardhi, wananchi wa Itilima wameiomba serikali kuwawekea uzio utakaowasaidia kuepukana na uvamizi wa mara kwa mara wa tembo wanaotoka hifadhini kwenda katika maeneo yao.
‘’Tunashukuru kwa ahadi ya kuwekewa uzio wa umeme kwa ajili ya kuzuia tembo kuvamia maeneo yetu ila tunaomba ahadi hiyo iwe ya kweli’. Amesema mkazi wa Itilima’
Hata hivyo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu amewaambia wananchi hao kuwa serikali tayari imejipanga kuhakikisha inajenga uzio wa umeme kwa ajili ya kuzuia tembo kuingia katika maeneo ya wananchi.
‘’Niwaase wananchi kutoenda katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kufanya uharibifu na mtoe ushirikiano wa kulinda uzio wa umeme pale utakaojengwa’’. Amesema
Mkuu wa wilaya ya Itilima Bi. Anna Gidarya amesema halmashauri ya wilaya ya Itilima ina lengo la kuandaa hati milki za viwanja vyote 1,604 vilivyopangwa ambapo hadi kufikia juni 2026 jumla ya hati milki 506 zimeandaliwa na kusajiliwa.
‘’Hati za viwanja vilivyosalia havijamilkishwa kwa vile wamiliki hawajalipia gharama za uandaaji wa milki hizo’’. Amesema Bi. Gidarya.
Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo amewataka wananchi wa Wilaya ya Itilima kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini kwa kuwa ndiyo msingi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amesema, hakuna uwekezaji unaoweza kufanyika kwa ufanisi katika mazingira yasiyo na amani, hivyo ni jukumu la wananchi kuendelea kuthamini na kulinda utulivu uliopo Tanzania.
Ameeleza kuwa maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, viwanda, biashara na miundombinu, yanahitaji mazingira tulivu yanayowawezesha wananchi na wawekezaji kufanya shughuli zao bila hofu.
“Uwekezaji wowote unategemea amani na utulivu na maendeleo yatakayopatikana yatatokana na amani. Hivyo amani inaiweka nchi katika nafasi nzuri ya kupokea wawekezaji,” amesema Dkt. Akwilapo.
Amesema uwepo wa amani unaifanya nchi kuwa na mazingira yanayovutia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo baadaye inaweza kutoa ajira, kuongeza mapato na kuboresha maisha ya wananchi.
Ziara ya Dkt Akwilapo wilayani Simiyu ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwapeleka mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa kwa wananchi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akilakiwa na wananchi wa Itilima alipowasili Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani itilima mkoa wa Simiyu kusikiliza kero za wananchi wakati wa ziara yake mkoani humo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akikabidhiwa Zawadi ya kuku na wananchi wa Kijiji cha Simiyu kata ya Migato mara baada ya kuzungumza nao wilayani Itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Daraja katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilaya ya Itilima mara baada ya kusikiliza kero za wananchi tarehe 7 Agosti 2026. Kulia kwa Dkt Akwilapo ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu mhe. Anamringi Macha na kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Itilima Bi. Anna Gidarya.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...