Na Said Mwishehe,Michuzi TV




MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA)imezindua Klabu za kupiga vita dawa za kulevya katika vyuo vikuu nchini ikiwani sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ushiriki wa jamii hususani wanafunzi wa vyuo vikuu katika kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya

Hatua ambayo pia inalenga kuimarisha kinga, kuongeza uelewa na kujenga mazingira yatakayosaidia vijana kufanya maamuzi salama na yenye tija kwa mustakabali wa maisha yao na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hizo leo Septemba 1,2026 katika ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo amesema vilabu hivyo vitatumika pia kutafakari kwa mtizamo wa kitaaluma kuhusu tatizo la dawa za kulevya.

Pia athari zake kwa vijana wa kizazi kipya kwani uraibu ni tatizo linalopoteza utu na kusababisha mateso kwa vijana. “Katika kubabiliana na tatizo hili, kunahitaji majibu ya kina na hatua za uzuiaji zinazohusisha jamii kikamilifu. Vilabu hivi vitatumika pia kwa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

“Tatizo la dawa za kulevya lina athari katika afya ya jamii, usalama, uchumi, familia na maendeleo ya Taifa. Kwa msingi huo, Serikali imeweka mikakati inayolenga kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya.”

Amefafanua mikakati hiyo ni kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya, uhitaji wa dawa za kulevya, madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

“Tukio lililotukutanisha leo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa pili wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya. Mkakati huu unasisitiza kinga kupitia elimu, uhamasishaji na hatua zinazolenga kuzuia watu kuanza kutumia dawa za kulevya.

“Katika utekelezaji wa mkakati huu, Mamlaka imeandaa muongozo wa utoaji elimu ambao umeainisha makundi yanayohitaji elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya. Wanafunzi wa Vyuo Vikuu ni miongoni mwa makundi hayo muhimu.

“Mamlaka imewalenga wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu mko katika mazingira ambayo yanahitaji uelewa sahihi na uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu masuala yanayoweza kuathiri afya, masomo na mustakabali wenu.

“Tumeshuhudia baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakishindwa kuendelea na masomo yao kutokana na makundi rika na kutumbukia kwenye starehe na matumizi ya dawa za kulevya,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Ameongeza pia vyuo vikuu ni vituo vya kuzalisha wataalamu na maarifa yanayosaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii. Kwa hiyo, elimu kuhusu dawa za kulevya inayotolewa kwa kundi hilo inalenga zaidi kuzuia matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi.

Amesisitiza lengo ni kujenga kizazi cha wataalamu kitakachoweza kulielewa tatizo hili kwa mtazamo wa kitaaluma na kulisaidia Taifa kupata suluhisho lenye ushahidi wa kisayansi ambalo linatumia akili mnemba (AI) na teknolojia katika kupunguza tatizo la dawa za kulevya nchini. Suluhisho la ubunifu wa kimkakati lenye tija kwa Taifa.

“Baada ya kupata elimu hii, Mamlaka inatarajia kuona wanafunzi na wataalamu wa vyuo vikuu wakishiriki katika tafiti kuhusu sababu na vihatarishi vya matumizi ya dawa za kulevya, mwenendo wa tatizo, madhara yake na ufanisi wa hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana nalo.

“Tafiti hizo zitasaidia kuongeza uelewa wa Taifa kuhusu tatizo hili na kutoa msingi wa kuboresha sera, mipango na afua za Serikali. Lipo ombwe la tafiti za kisayansi na kitaaluma juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa ujumla,”

Amesema hivyo anawahamasisha wanataaluma kujikita kwenye tafiti ili kupata majibu ya kisayansi na kitaaluma juu ya tatizo la dawa za kulevya.”Ninyi kama wataalamu wa afya, mtasaidia katika tafiti kuhusu madhara ya kiafya na tiba…

“Watalaam wa saikolojia na jamii wanaweza kuchunguza sababu zinazochochea matumizi, wataalamu wa sheria wanaweza kusaidia katika kuchambua changamoto za utekelezaji wa sheria huku wataalamu wa TEHAMA wakichangia matumizi ya teknolojia katika kupunguza uingiaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya”

Awali Mwakilishi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu) Tanzania (TAHILISO) Aron Seni amesema vyuo hivyo ni vituo muhimu vya kuzalisha wataalamu na viongozi wa kesho.

Amefafanua lakini mazingira ya sasa yanaweza kuwaweka vijana katika hatari ya kushawishika kutumia dawa za kulevya kutokana na uhuru wa maisha ya chuoni, shinikizo kutoka kwa marafiki na changamoto za maisha.

“Tumeshuhudia baadhi ya vijana kutoka taasisi za elimu ya juu wakikamatwa, kufunguliwa mashtaka na wengine kuhukumiwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya,” amesema.

Ameongeza baadhi ya wanafunzi huanza kutumia dawa hizo kwa majaribio, kushawishiwa na marafiki au kutokana na changamoto mbalimbali za maisha, hivyo hatua za mapema za kinga na elimu zinahitajika.

Amesisitiza klabu hizo hazipaswi kuwa vikundi vya kufanya shughuli za kawaida au kupiga picha kwa ajili ya mitandao ya kijamii, bali ziwe nguzo za elimu, ulinzi na ukombozi wa vijana.

“Klabu hizi zitatoa nafasi salama kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya kupata elimu, ushauri na msaada bila kuhukumiwa.Tunaishukuru DCEA kwa ushirikiano uliowezesha kufanikisha mchakato huu.”











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...