Na Janeth Raphael - MichuziTv
Malezi ya mtoto katika hatua za awali za maisha yana nafasi kubwa katika kujenga tabia, mwenendo na mustakabali wake, huku ukosefu wa uangalizi na malezi bora ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuwafanya watoto kukua katika mazingira hatarishi na kujihusisha na vitendo visivyofaa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Nusu ya Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Dkt. Gwajima amesema baadhi ya wazazi wanapopata watoto hawatoi malezi na mwelekeo unaostahili, hali ambayo huwa mbaya zaidi pale wazazi wanapotengana na watoto kuachwa bila uangalizi wa kutosha, hivyo kuwalazimu baadhi yao kujilea wenyewe katika mazingira ya mitaani.
Amesema malezi ya mtoto yanapaswa kuanza kwa maandalizi na makubaliano ya wazazi kabla ya kupata watoto, huku akisisitiza kuwa jukumu la malezi halipaswi kuachwa kwa mzazi mmoja pekee, bali linahitaji ushirikiano wa familia na jamii nzima ili kuhakikisha mtoto anakua katika mazingira salama na yenye mwelekeo sahihi.
Dkt. Gwajima, amesema uwekezaji katika maendeleo ya binadamu huanza tangu hatua za mwanzo kabisa za maisha, hivyo ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata malezi, makuzi na huduma stahiki katika umri wao wa awali, ikiwa ni pamoja na kupitia familia, jamii na vituo vinavyotoa huduma za malezi ya watoto.
Aidha, amewataka waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuelimisha na kuhamasisha wazazi na wananchi kuhusu umuhimu wa malezi bora, akisisitiza kuwa mtoto anayejengewa misingi imara tangu utotoni anaandaliwa kuwa sehemu muhimu ya kizazi kinachojitambua na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Amesema, kama ilivyo kwa nyumba inayohitaji msingi imara ili iweze kudumu, ndivyo maisha ya mtoto yanavyohitaji msingi mzuri wa malezi tangu mwanzo.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...