Na Janeth Raphael – MichuziTv

Serikali imeeleza kuwa pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji hatua endelevu, ikiwemo migongano kati ya binadamu na wanyamapori, ujangili, uvamizi wa maeneo ya hifadhi na shoroba pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amesema hayo leo Septemba 11, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo kwa marubani wa ndege nyuki (drones) na kukabidhi vitendea kazi, iliyofanyika Mtumba, Dodoma.

Dkt. Kijaji amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori, lakini ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori bado ni changamoto inayohitaji kupewa kipaumbele kutokana na madhara inayosababisha kwa wananchi, mifugo na mazao.

Amesema matukio hayo yanaweza pia kuathiri mtazamo wa jamii kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, hivyo Serikali inaendelea kutafuta njia bora za kuzuia na kudhibiti migongano hiyo kabla haijasababisha madhara makubwa kwa wananchi.

Dkt. Kijaji amesema ujangili na biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu ni miongoni mwa changamoto nyingine zinazoendelea kuhatarisha uwepo wa baadhi ya spishi za wanyamapori na uendelevu wa rasilimali za asili.

Amesema upanuzi wa shughuli za kibinadamu, ikiwemo kilimo, ufugaji, uchimbaji wa madini na ujenzi wa makazi katika maeneo yasiyozingatia mipango bora ya matumizi ya ardhi, umeongeza shinikizo katika maeneo ya hifadhi na kutishia kupotea kwa baadhi ya makazi muhimu ya wanyamapori.

Aidha, amesema uvamizi wa shoroba za wanyamapori umeendelea kuwa kikwazo kwa uhamaji wa wanyamapori kutoka eneo moja kwenda jingine, hali inayoweza kuathiri mifumo ya ikolojia inayounganisha maeneo mbalimbali ya hifadhi.

Dkt. Kijaji ametaja pia kuenea kwa mimea vamizi ndani ya maeneo ya hifadhi kuwa changamoto inayopunguza ubora wa makazi na malisho ya wanyamapori, huku mabadiliko ya tabianchi yakichangia ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, upungufu wa maji na uharibifu wa miundombinu ya uhifadhi.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kitaifa kwa kushirikiana na wananchi na wadau wa uhifadhi, huku ikiongeza matumizi ya teknolojia katika kuboresha usimamizi na ulinzi wa rasilimali hizo.

Dkt. Kijaji amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara imeweka kipaumbele katika kupunguza migongano ya binadamu na wanyamapori kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Utatuzi wa Migongano ya Binadamu na Wanyamapori wa Miaka 10.

Amesema mkakati huo unalenga kuzuia, kudhibiti na kushughulikia kwa haraka matukio yanayohusisha wanyamapori wakali na waharibifu, ili kupunguza madhara kwa wananchi na kulinda usalama wa jamii.

Ametaja pia Mkakati wa Usimamizi na Uhifadhi wa Tembo wa Miaka 10, unaolenga kuimarisha uhifadhi endelevu wa tembo pamoja na kupunguza athari hasi dhidi ya wanyama hao na makazi yao.

Vilevile, Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kuongoa na Kurasimisha Shoroba za Wanyamapori wa Miaka Mitano, unaolenga kuimarisha hali ya uhifadhi katika maeneo yanayotumiwa na wanyamapori wanapohama kutoka hifadhi moja kwenda nyingine au kutoka nchi moja kwenda nyingine ndani ya mifumo ikolojia inayovuka mipaka.

Amesema mfumo huo unasaidia mamlaka kupata taarifa kwa haraka na kuchukua hatua za kudhibiti matukio hayo, sambamba na kurahisisha mchakato wa ulipaji wa kifuta jasho au kifuta machozi kwa wananchi walioathirika.

Dkt. Kijaji amesema matumizi ya ndege nyuki (drones) nayo yanaendelea kupewa umuhimu katika ufuatiliaji na usimamizi wa maeneo ya uhifadhi, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa taarifa na kuwezesha hatua kuchukuliwa kwa wakati dhidi ya changamoto zinazojitokeza.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya uhifadhi hayawezi kutegemea Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wananchi na wadau wa uhifadhi ili kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa, zinatunzwa na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...