Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu ni muhimu katika kuokoa maisha ya mama, watoto wachanga na watoto, na kuchangia ujenzi wa afya bora, nguvu kazi na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mhe. Ndejembi amesema hayo Septemba 23, 2026 jijini New York, Marekani, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu kwa ajili ya uhai wa mama na mtoto barani Afrika.

Mkutano huo uliandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Amesema Afrika bado inakabiliwa na kiwango kikubwa cha vifo vya kina mama na watoto licha ya hatua mbalimbali za maendeleo zilizopigwa katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi, Afrika inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani na karibu theluthi mbili ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, huku sehemu kubwa ya vifo hivyo ikiwa inaweza kuzuilika.

Amesema Ajenda ya Sifuri Tatu inalenga kufikia sifuri ya kujifungua nyumbani bila msaada wa mtaalamu mwenye ujuzi, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto mchanga, na sifuri ya watoto wasiopata chanjo.

Mhe. Ndejembi amesema kufikia malengo hayo kunahitaji kuimarishwa kwa huduma za afya ya msingi, kuongezwa kwa wataalamu wenye ujuzi, kuboreshwa kwa mifumo ya rufaa, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu, pamoja na kuhakikisha fedha zinafika katika ngazi ya utoaji huduma.

Aidha, amesema Tanzania imeendelea kujenga uzoefu katika kuimarisha huduma za afya ya msingi na huduma za dharura kwa mama na mtoto mchanga, ikiwemo mfumo wa rufaa wa kidijitali wa m-Mama, pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa vifo vya kina mama na watoto.

Amesema uzoefu huo unaonesha umuhimu wa kuunganisha uongozi wa kisiasa, uwekezaji na utekelezaji wenye uwajibikaji ili kuboresha matokeo ya afya na kuhakikisha huduma zinazookoa maisha zinawafikia wananchi kwa wakati.

Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa viongozi barani Afrika kuimarisha uwajibikaji wa kisiasa, kuongeza uwekezaji katika huduma zinazookoa maisha na kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinafanyiwa kazi hadi katika ngazi ya utekelezaji.

“Hakuna mwanamke anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa usafiri, damu au huduma yenye ujuzi, wala mtoto anayepaswa kupoteza maisha kwa kukosa huduma inayoweza kuokoa maisha au chanjo,” amesema.

Amesisitiza kuwa kaulimbiu “Jiongeze Tuwavushe Salama” ni wito wa kuchukua hatua kwa ajili ya kuhakikisha kila mama, mtoto mchanga, mtoto na kijana anapata fursa ya kuishi na kukua katika mazingira yenye afya bora.















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...