Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuwa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) kwa mwaka 2026 utafanyika Septemba 9 na 10, ukihusisha watahiniwa 1,168,649 kutoka shule 20,019 nchini.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said A. Mohamed, amesema kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 531,467 sawa na asilimia 45, huku wasichana wakiwa 637,182 sawa na asilimia 55.
Amesema watahiniwa 1,081,204 sawa na asilimia 93 watafanya mtihani kwa Kiswahili, huku 87,445 sawa na asilimia saba wakifanya kwa lugha ya Kiingereza.
Kwa mujibu wa Prof. Mohamed, watahiniwa wenye mahitaji maalumu 4,867 pia wamesajiliwa kufanya mtihani huo. Kati yao, 82 ni wasioona, 1,591 wenye uoni hafifu, 999 wenye uziwi, 576 wenye ulemavu wa akili na 1,619 wenye ulemavu wa viungo.
Amesema masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili.
Prof. Mohamed amesema mtihani huo ni wa mwisho kufanyika kwa kutumia mtaala wa sasa, huku ukilenga kupima maarifa na ujuzi walioupata wanafunzi katika miaka saba ya elimu ya msingi na kutumika katika mchakato wa uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari.
Amesema maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika, yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani na nyaraka muhimu katika halmashauri zote nchini, mafunzo kwa wasimamizi pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa vituo vya mitihani.
Amewataka wasimamizi wa mitihani kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia kanuni za mitihani, huku wakihakikisha watahiniwa wote wanapata fursa ya kufanya mtihani kwa muda uliopangwa.
Kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu, amesema NECTA imeweka utaratibu wa kuwapatia maandishi ya nukta nundu kwa wasioona, maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu na muda wa ziada wa dakika 20 kwa kila saa katika somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine.
Aidha, amewataka watahiniwa kuepuka vitendo vya udanganyifu, akisisitiza kuwa matokeo ya mwanafunzi atakayebainika kufanya udanganyifu yatafutwa kwa mujibu wa kanuni.
Amewataka wamiliki na wakuu wa shule kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wakati wa mtihani, akionya kuwa NECTA inaweza kufuta kituo cha mtihani endapo itabaini uwepo wake unahatarisha usalama wa mtihani.
Pia ameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha mitihani inafanyika kwa amani na utulivu, ikiwemo kuheshimu maeneo ya mitihani na kuepuka kuingia shuleni wakati wa uendeshaji wa mtihani.
NECTA imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya udanganyifu kupitia namba 0759 360 000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz.
Mtihani huo utafanyika Jumatano, Septemba 9, na Alhamisi, Septemba 10, 2026.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...