Na Mwamvua Mwinyi, Pwani


MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewaagiza wafugaji mkoani humo kuacha mara moja kuingiza na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo.

Nyongo alitoa agizo hilo Septemba 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri za Mji wa Rufiji na Kibiti, ambako alisikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukuliwa.

Alisema Serikali haiwezi kuendelea kushuhudia mazao ya wakulima yakiharibiwa na mifugo, wakati maeneo yametengwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

“Hatukubali kuendelea kuona mazao ya wakulima yakiharibiwa wakati kila kundi limetengewa maeneo kwa ajili ya shughuli zake. Wafugaji waheshimu maeneo ya wakulima na waache mara moja kuingiza mifugo kwenye mashamba,” alisema.

Aidha, alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha wafugaji watakaobainika kuingiza au kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Nyongo aliipongeza Halmashauri ya Rufiji kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka malengo yaliyowekwa, huku akizitaka Halmashauri za Rufiji na Kibiti kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato ili kuongeza uwezo wa Serikali za mitaa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kuhusu utabiri wa mvua kubwa za msimu wa Vuli unaohusishwa na hali ya El Niño, Nyongo alizitaka halmashauri hizo kuimarisha maandalizi na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi kuhama mapema na kuhamia maeneo salama, akisisitiza kuwa usalama wa maisha ya wananchi unapaswa kupewa kipaumbele.

Pia, aliwataka Wakuu wa Wilaya za Rufiji na Kibiti kutambua na kuainisha maeneo salama yatakayotumika kuwaweka wananchi watakaoweza kuathiriwa na mvua hizo, pamoja na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika maeneo hayo.

Ziara hiyo ni ya kwanza ya kikazi kwa Nyongo katika halmashauri hizo tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ikiwa na lengo la kujitambulisha, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...