Na Jane Mwakyoma - Rukwa
MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imewakutanisha wadau mbalimbali mkoani Rukwa wakiwemo watoa huduma za mawasiliano ya simu, sekta ya usafiri, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii, kwa lengo la kujadili namna ya kukabiliana na kutokomeza uhalifu wa mtandaoni unaoendelea kushika kasi mkoani humo.
Akifungua mkutano huo jana kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Rukwa mkuu wa wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa na kuripoti vitendo vya uhalifu wa mtandaoni, ikiwemo kuwabaini na kuwafichua wahalifu waliopo katika maeneo yao.
"Tushirikiane kwa pamoja katika kutokomeza uhalifu wa mitandaoni Rukwa bila matukio haya inawezekana nguvu ya pamoja inahitajika." Amesema Lijualikali.
kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa TCRA mhandisi Peter Mwasalyanda amesema bado kuna mwendelezo wa vitendo vya uhalifu vinavyofanyika kupitia huduma za simu na intaneti, huku mkoa wa Rukwa ukiendelea kukabiliwa na changamoto hiyo.
Amesema juhudi za kudhibiti vitendo hivyo zinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya TCRA, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na jamii.
Akitoa takwimu mhandisi Mwasalyanda amesema mkoa wa Rukwa una jumla ya matukio 1330 kwa wilaya ya Sumbawanga, Kalambo 612, na wilaya ya Nkasi matukio 553.
Amesisitiza kuwa mafanikio katika kudhibiti uhalifu wa mtandaoni yanategemea ushirikiano wa wadau wote, kila mmoja akitimiza wajibu wake katika kuzuia na kupambana na vitendo hivyo.
Amesema TCRA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu na kuchukua hatua zinazolenga kuimarisha usalama wa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
Aidha, wadau mbalimbali walioshiriki mkutano huo, wakiwemo viongozi wa dini, wamesisitiza umuhimu wa elimu, malezi bora na maadili mema katika jamii, hususan kwa watoto, ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kujiepusha na vitendo vya uhalifu wa mtandaoni.
" Ni muhimu elimu ikatolewa kwa wananchi hasa waishio vijijini ili wawe na uelewa wa kutosha kwa kuwa wao ni wahanga wa matukio hayo " mmoja wa wadau amesema.






.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...