-Yazindua bidhaa tatu za Jubilee Life Insurance ambazo ni Fanaka Plus, Smart Education Insurance Plan na Akiba Flex Plan


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezitaka kampuni za bima kubuni bidhaa zinazotoa majibu ya vitendo kwa changamoto zinazowakabili wananchi, ikisema ubora wa bidhaa za bima haupaswi kupimwa kwa idadi ya watu waliojiunga pekee.

Kamishna wa Bima, Dk.Baghayo Saqware amesema kampuni zinazolenga kuongeza ujumuishi wa kifedha zinapaswa kwanza kuelewa mazingira wanamoishi Watanzania na changamoto zinazowakabili kabla ya kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji yao.

Dk.Saqware ametoa kauli hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Uzingatiaji wa Sheria na Kanuni wa TIRA, Bw Alex Rock wakati wa uzinduzi wa bidhaa tatu mpya za bima ya maisha za Jubilee Life Insurance Tanzania uliofanyika leo Septemba 3,2026 jijini Dar es Salaam.

“Mwito wangu kwa Jubilee Life Insurance na kampuni nyingine za bima ni kuendelea kubuni bidhaa zinazotoa majibu kwa changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao,” amesema Dk Saqware.

“Ubora wa bidhaa haupimwi kwa idadi ya watu waliojiunga pekee. Uelewa hujenga imani, na imani huongeza matumizi endelevu ya bima,”amesema na kuongeza Tanzania inaingia katika hatua muhimu ya kujenga familia zenye uwezo wa kustahimili misukosuko ya kifedha na taifa lenye uimara wa kifedha huku bima ya maisha ikiwa na nafasi muhimu katika kulinda wananchi na kusaidia mipango yao ya muda mrefu.

Katika hafla hiyo, Dk.Saqware amezindua bidhaa tatu za Jubilee Life Insurance ambazo ni Fanaka Plus, Smart Education Insurance Plan na Akiba Flex Plan, zilizobuniwa kusaidia wananchi katika uwekaji akiba, maandalizi ya elimu, ulinzi wa maisha na mahitaji mengine ya kifedha ya baadaye.

Ameongeza Jubilee Life Insurance kwa kuwasilisha bidhaa hizo kwa lugha ya Kiswahili, akisema matumizi ya lugha inayoeleweka kwa urahisi ni muhimu katika kuongeza uelewa na ujumuishi katika huduma za bima.

“Matumizi ya lugha inayoeleweka katika kutoa taarifa na elimu kuhusu bima huwawezesha wananchi kuelewa kwa usahihi faida, masharti na wajibu wao kabla na baada ya kujiunga na bima,” alisema.

Dk.Saqware amesema pia bima ya maisha ni nyenzo muhimu katika kujenga usalama wa kifedha na uwezo wa kustahimili changamoto kwa mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

Amesisitiza bima hiyo hulinda kipato na mipango ya maisha dhidi ya athari za kifo, ulemavu, maradhi, ajali na matukio mengine yasiyotarajiwa, huku pia ikiwasaidia wananchi kuweka akiba kwa ajili ya mahitaji muhimu ya baadaye, yakiwemo elimu ya watoto na ustawi wa familia.

“Bila ulinzi wa bima, tukio lisilotarajiwa linaweza kukatisha elimu ya watoto, kuathiri maisha ya familia na hata kuzima ndoto za wanufaika,” alisema.Kupitia bima ya maisha, ndoto na mipango hiyo inaweza kulindwa na kuendelea kuwa halisi.”

Pia amesema matumizi ya bima ya maisha nchini bado hayajafikia kiwango kinachotarajiwa, huku baadhi ya sababu zikitajwa kuwa ni aina na muundo wa bidhaa zinazopatikana sokoni pamoja na uwezo wake wa kujibu mahitaji halisi ya wananchi.

Pamoja na hayo amesema uzinduzi wa bidhaa hizo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko.

Amesema hatua hiyo pia inaunga mkono Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020–2030, ambao unalenga kuongeza mchango wa bima ya maisha katika pato la taifa hadi kufikia asilimia 3 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance Tanzania Helena Mzena amesema kampuni hiyo imeendelea kuboresha bidhaa zake ili kuwapatia wateja thamani na uhakika zaidi.

Amesema Fanaka Life Plan imeboreshwa na kubadilishwa jina kuwa Fanaka Plus, ikiwapa wateja fursa ya kukuza fedha zao huku wakipata ulinzi wa maisha na amani ya moyo.

Ameongeza kuwa Akiba Flex inawapa wateja uhuru zaidi wa kuweka michango na kufanya miamala ya fedha kulingana na mahitaji yao.

Aidha, amesema Smart Education Insurance Plan imeundwa mahsusi kuwasaidia wazazi na walezi kujiandaa kwa ajili ya elimu ya watoto wao.“Hapa, mteja anaweza kuweka akiba ili kuhakikisha ndoto za kielimu za watoto wake zinatimia, huku pia akiwa na ulinzi wa maisha.

“Bidhaa hizi za bima ni ushahidi kwamba tunajali na kuthamini ndoto za wateja wetu na tunataka kuhakikisha ndoto hizo zinatimia bila msongo usio wa lazima.”

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Jubilee Insurance Amyn Lalji amesema uzinduzi huo ni hatua nyingine muhimu katika safari ya Jubilee Life Insurance Tanzania na unaakisi dhamira ya kampuni hiyo ya kutoa suluhisho bunifu na la vitendo linalokidhi mahitaji yanayobadilika ya Watanzania.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...