Na Nasra Ismail, Geita

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea kuvutia wawekezaji wa kigeni nchini kutokana na maboresho ya mazingira ya uwekezaji yanayofanywa na Serikali, huku wawekezaji hao wakieleza kuridhishwa na sera na vivutio vinavyotolewa.

Hayo yamebainika wakati viongozi wa TISEZA wakiongozwa na Mjumbe wa Bodi, Absalom Kibanda, walipotembelea Mgodi wa Jiuding Mining mkoani Geita, na kujionea shughuli za uwekezaji zinazofanywa na kampuni hiyo.

Kibanda amesema wamefurahishwa na namna mwekezaji huyo alivyojikita katika uwekezaji nchini pamoja na ushirikiano wake na wazawa, akieleza kuwa uwekezaji huo umekuwa na manufaa kwa jamii.

"Uwekezaji huu umetoa ajira kwa Watanzania na kuwapatia wazawa msaada wa kitaalamu unaowawezesha kuongeza ujuzi katika maeneo mbalimbali ya kazi," amesema Kibanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mgodi huo, Ju Liu, raia wa China, amesema alipofika nchini mwaka 2021 alipata ushauri katika ofisi za TISEZA kuhusu maeneo mbalimbali ya uwekezaji, na kupitia ushauri huo aliamua kuwekeza katika sekta ya madini.

Ju Liu amesema licha ya kuwekeza madini, ana mpango wa kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha sukari nchini, akivutiwa na sera nzuri na mazingira ya kodi yaliyowekwa na Serikali, ikiwemo utaratibu wa kupunguziwa baadhi ya kodi kwa vitu vinavyoagizwa kutoka nje kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema kupitia mgodi huo, kampuni yake imeweza kutoa ajira kwa Watanzania 73 ambao wamekuwa wakinufaika kiuchumi.

Naye mfanyakazi wa kampuni hiyo, Dotto Bahati, amesema uwepo wa mgodi huo umekuwa na msaada mkubwa kwao kutokana na ajira na maslahi mazuri wanayoyapata, ambayo yamewasaidia kuboresha maisha yao na kutimiza majukumu ya kifamilia na kijamii.

Wawekezaji hao wamesema uwekezaji katika sekta ya madini umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa, huku mazingira rafiki ya uwekezaji yakisaidia wawekezaji kuanzisha na kuendeleza shughuli zao nchini.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...