SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27 litaelekeza nguvu, rasilimali fedha na wataalamu wake katika kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa gesi asilia, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini na katika nchi jirani.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alisema hayo jana, Septemba 21, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Shirika kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mipango yake kwa mwaka 2026/27.
Alisema TPDC itaendelea kuongeza uzalishaji wa gesi katika Vitalu vya Mnazi Bay na Songo Songo, huku ikielekeza nguvu zaidi katika Kitalu cha Ruvuma, hususan eneo la Ntorya, ambako shughuli za uendelezaji wa gesi iliyogunduliwa zinaendelea.
Kwa mujibu wa Makame, Shirika linatarajia pia kukamilisha ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya hadi Madimba, hatua inayolenga kuwezesha matumizi zaidi ya rasilimali hiyo.
Katika eneo la utafutaji wa mafuta na gesi, alisema TPDC itaendelea na shughuli katika vitalu vyake vya kimkakati, ikiwemo Lindi-Mtwara, ambako ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za mtetemo za 3D unaendelea.
Alisema katika Kitalu cha Eyasi Wembere, hatua za mwisho za ukusanyaji wa taarifa za mtetemo za 2D zinaendelea kabla ya maandalizi ya taarifa za 3D na uchimbaji wa visima vya utafutaji.
Aidha, shughuli za ukusanyaji wa taarifa za mtetemo za 3D zitaendelea katika Kitalu cha Songo Songo Magharibi, huku katika Kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini, TPDC ikiendelea kutafuta wabia wa kimkakati kwa ajili ya uchimbaji wa visima vya utafutaji.
Makame alisema sambamba na kuongeza uzalishaji, TPDC itaendelea kupanua matumizi ya gesi asilia kwa kuwaunganisha wateja wapya, wakiwemo viwanda, taasisi na kaya.
Alisema Shirika pia litaendelea kuhakikisha gesi inafikishwa katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mabomba na teknolojia mbadala, ikiwemo Mini-LNG na CNG.
Katika miundombinu ya usafirishaji wa gesi, alisema mkazo utawekwa katika kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Kinyerezi hadi Chalinze.
Katika hatua nyingine, TPDC itaendelea kusimamia na kuongeza tija katika kampuni zake tanzu, ikiwemo GASCO na TANOIL, huku ikiendeleza mpango wa kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa kitovu cha biashara ya mafuta.
Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na UNOC na Vitol Bahrain, unahusisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi (Refinery), miundombinu ya kuhifadhi mafuta ghafi na yaliyosafishwa, mabomba ya kusafirisha mafuta pamoja na miundombinu mingine wezeshi.
Makame alisema kufuatia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano (MoU), timu za kuratibu mradi huo zimeundwa na zimeanza kutekeleza majukumu mbalimbali.
Kwa upande wa Taifa, alisema uwekezaji katika utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi unaendelea kufungua fursa za ajira, biashara, ujuzi na matumizi ya teknolojia, sambamba na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika sekta hiyo.
Aidha, TPDC imewataka vijana kuendelea kujitayarisha kushiriki katika sekta ya mafuta na gesi, ambayo inahitaji nguvu kazi yenye ujuzi na utaalamu mbalimbali.
Shirika hilo limesisitiza kuwa litaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi asilia zinatumika kwa tija, uwazi na kwa manufaa mapana ya Taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...