WAZIRI wa Madini, Mafuta na Nishati wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mateka Mufuwa Simplice, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utayari wake wa kushirikiana na DRC katika kuimarisha udhibiti wa upotevu wa mapato ya Serikali, hususan kupitia upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa za mizigo inayoingia DRC kupitia Tanzania.

Simplice ameyasema hayo leo, Septemba 21, 2026, katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa DRC mkoani Kigoma, kati ya Ubalozi huo na TRA Mkoa wa Kigoma, kwa lengo la kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini DRC, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiutawala kati ya Tanzania na DRC.

Akizungumza katika kikao hicho, Simplice alisema tofauti na kutokulingana kwa taarifa zilizomo katika nyaraka za usafirishaji wa mizigo (manifest documents) ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri upatikanaji wa taarifa sahihi za mizigo na hivyo kuwa na athari katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ya DRC. Alieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka husika za Tanzania na DRC, hususan katika ubadilishanaji wa taarifa za mizigo, unaweza kusaidia kuimarisha uwazi, ufuatiliaji na udhibiti wa mizigo inayopita katika njia za biashara kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Beatus Nchota, alisema TRA iko tayari kuendelea kushirikiana na mamlaka za DRC katika kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa mizigo inayopita Tanzania kuelekea DRC, pamoja na mizigo inayosafirishwa moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda nchini humo.


Nchota alipendekeza kuwa DRC itumie fursa za ushirikiano zilizopo kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususani ushuru wa pamoja, kwa kufungua ofisi na uwepo wa maafisa wa Forodha hapa nchini Tanzania ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mizigo kwa wakati, pamoja na kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa mizigo inayopita Tanzania kuelekea DRC.

Aidha, Nchota aliwakaribisha maafisa wa Forodha wa DRC kutembelea Tanzania na kujifunza kuhusu taratibu na mifumo inayotumika katika uingizaji, usafirishaji na udhibiti wa bidhaa, hatua ambayo itasaidia kuongeza uelewa wa pamoja na kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa kuhusu mizigo inayoingia nchini DRC kupitia Tanzania.

Kikao hicho kimeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa mipaka na biashara, hususan katika kuboresha ubadilishanaji wa taarifa, kuimarisha udhibiti wa mizigo na kusaidia nchi zote mbili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...