Na John Mapepele – WAF New York

WAZIRI wa Afya, Mhe. Mohamed  Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje, kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Mhe. Mchengerwa amebainisha hayo leo, jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika kikao cha ‘Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028’, ambapo ameiwakilisha Tanzania akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Grace Magembe katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.

Kikao hiki ambacho kimeratibiwa  na Serikali ya  Sierra Leone kinafanyika pembezoni mwa  Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika kikao cha 81 (UNGA 81), unaowakutanisha wawakilishi wa nchi zote 193 wanachama wa UN na kila nchi ina kura moja ambapo kwa Tanzania, Makamo wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi anamwakilisha Rais,  Mhe Rais Samia Suluhu  kuongoza ujumbe wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo Mhe.Mchengerwa amefafanua kuwa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030 unaolenga kufikia malengo ‘zero tatu’, ambayo ni kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani na usio na wataalamu, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.

“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero tatu,” amesisitiza  Mhe. Mchengerwa.

Aidha, ameeleza kuwa  Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana jirani na wananchi wote nchi nzima  pia Serikali inaimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto na kuwalinda wananchi dhidi ya gharama kubwa za matibabu.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa Serikali  inaendelea kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, ufadhili wa moja kwa moja wa vituo vya kutolea huduma za afya, mifumo ya malipo ya kielektroniki, tozo zinazolenga bidhaa maalum pamoja na kuendeleza huduma za utalii tiba, huku ikiendelea kuongeza mgao wa bajeti kwa huduma za afya ya msingi na huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga.

Akizungumzia umuhimu wa uzalishaji wa ndani, amesema Afrika hutumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 28 kila mwaka kununua dawa na bidhaa za afya, huku sehemu kubwa ya mahitaji hayo ikitoka nje ya bara hilo, jambo alilosema linaweka mifumo ya afya katika hatari ya kukumbwa na changamoto za misukosuko ya minyororo ya usambazaji na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa.

Amesema Tanzania imeweka uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya, vifaa tiba na vifaa vya hospitali kuwa kipaumbele cha kitaifa, akisisitiza kuwa hatua hiyo si suala la uchumi pekee bali pia ni msingi wa kuimarisha usalama wa afya kwa kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinaendelea kuwa na mahitaji muhimu hata pale kunapokuwa na changamoto katika minyororo ya usambazaji duniani.

Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo kuunganisha nguvu katika uwekezaji wa sekta ya afya, uhamishaji wa teknolojia na sera za viwanda ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, kuimarisha mamlaka za udhibiti na kuunga mkono ubunifu unaozalishwa barani Afrika. 

"Tanzania inaendelea  kuhakikisha huduma muhimu za afya zinapatikana ndani ya umbali usiozidi kilomita tano kutoka kwa kila jamii, huku hospitali za rufaa zikitumika zaidi kwa wagonjwa wenye mahitaji ya huduma maalum" amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Viongozi wa nchi  wanachama wa jumuiya hii hutumia jukwaa hili kueleza misimamo na vipaumbele vyao kuhusu masuala ya kimataifa.

Katika mkutano wa mwaka huu mambo yanayojadiliwa ni pamoja na amani na usalama, vita na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, AI, afya ya dunia , maendeleo na SDGs. 

Kaulimbiu ya UNGA 81 ni (Restoring Trust, Managing Transformation), Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...