Mwamvua Mwinyi, Pwani


WAKULIMA mkoani Pwani wametakiwa kuendelea kuandaa mashamba na kupanda mazao mbalimbali, yakiwemo yanayostahimili unyevu na mvua nyingi, huku wakizingatia ushauri wa wataalamu kutokana na utabiri wa mvua za msimu wa Vuli unaotarajiwa kuathiriwa na hali ya El NiƱo.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Ofisa wa Hali ya Hewa mkoani Pwani kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mussa Nkucha, kufuatia utabiri wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.

Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mbalimbali, hali inayoweza kuambatana na unyevu mwingi ardhini pamoja na uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.

Mussa amewataka wakulima kupanda mazao kwa wakati kwa kuzingatia tarehe za kuanza kwa mvua katika maeneo yao, ambazo zinatarajiwa kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi Oktoba mwaka huu.

Aidha, amewashauri wakulima kuchimba mifereji ya kupitisha maji ya ziada na kuweka matuta kinga ili kudhibiti maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda rutuba ya mashamba.

Pia amewataka kutumia mbinu na teknolojia zinazosaidia kuzuia maji kutuama mashambani, hali ambayo inaweza kusababisha mizizi ya mazao kuoza, pamoja na kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ili maji ya ziada yaweze kutumika katika vipindi vya ukavu au msimu unaofuata.

“Wakulima wawasiliane kwa karibu na Maafisa Ugani katika maeneo yao ili kupata ushauri unaozingatia aina ya udongo, mazao na hali ya hewa ya maeneo yao,” amesema.

Vilevile, amewataka wakulima na wananchi kwa ujumla kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa kila siku ili waweze kuchukua hatua stahiki kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...