Watu wawili wamefariki na askari wanne wa Jeshi la Polisi wamejeruhiwa katika vurugu zilizotokea baada ya tukio la mauaji katika eneo la Tindiga, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro leo Septemba 24, 2026 tukio hilo lilitokea Septemba 23, 2026, majira ya saa 7:00 mchana katika eneo la Mashamba ya Bondeni, Kitongoji cha Legeza Mwendo, Kijiji cha Malangali, Kata ya Tindiga.

Taarifa hiyo imesema Festo Selias Chaula, maarufu Walter, mkulima na mkazi wa Tindiga, alijeruhiwa baada ya kukatwa kichwani kwa kitu chenye makali na kupigwa kwa vitu butu sehemu mbalimbali za mwili.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza kuwafuatilia na kuwakamata watu waliodaiwa kuhusika kabla ya kuwapeleka Kituo cha Polisi Kilosa kwa mahojiano.

Hata hivyo, wakati watuhumiwa hao wakisafirishwa na askari kwa gari la Polisi aina ya Toyota Hilux pamoja na pikipiki tatu, kundi la watu lilifika eneo hilo na kuanza kuwashambulia askari na watuhumiwa.

Kwa mujibu wa Polisi, watu hao waliodaiwa kuwa wanachama wa chama cha wakulima walitumia silaha mbalimbali za jadi, zikiwemo visu, mapanga, mishale, mikuki, marungu na mawe.

Katika vurugu hizo, askari wanne walijeruhiwa, huku Polisi ikitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo.

Katika vurugu hizo Kelvin Mhagama, mkulima na mkazi wa Kichangani, alijeruhiwa na kitu chenye makali na baadaye alifariki akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.

Vurugu hizo pia zilisababisha uharibifu wa mali za Polisi, ambapo pikipiki yenye namba PT 3131, aina ya SANLG, ilichomwa moto na kuteketea. Gari la Polisi aina ya Toyota Hilux, lenye namba PT 5877, nalo liliharibiwa baada ya kupigwa kwa mawe.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...