Ifakara, Morogoro. Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imekabidhi vifaa tiba na vifaa vya kujifungulia katika Kituo cha Afya Kibaoni, Ifakara, ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni ya Tumaini inayolenga kuunga mkono huduma za afya kwa mama mjamzito.

Kituo hicho kinakuwa cha pili kunufaika na kampeni hiyo iliyoanzishwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kupitia mchango wa wafanyakazi wa Yas.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia, viti mwendo, mashuka, khanga, aproni pamoja na vifaa muhimu vinavyotumika wakati wa kujifungua (maternity kits).

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dustan Kyobya, amepongeza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya, akisema mchango wa wadau una nafasi muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika huduma za mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini, Joseph Mutalemwa, amesema Kampeni ya Tumaini ilitokana na uamuzi wa wafanyakazi wa kampuni hiyo kuunganisha nguvu na kutoa mchango unaogusa moja kwa moja mahitaji ya jamii.

“Tunatambua kuwa ujio wa mtoto duniani ni wakati wa furaha na matumaini kwa kila familia, lakini pia ni kipindi ambacho mama anahitaji huduma bora, uangalizi wa karibu na mazingira salama ya kujifungua. Msaada huu ni sehemu ya kuunga mkono huduma za uzazi zinazotolewa hapa Kibaoni,” amesema Mutalemwa.

Amesema pamoja na jukumu la Yas la kuwaunganisha Watanzania kupitia huduma za mawasiliano, kampuni hiyo inaona umuhimu wa kushiriki katika juhudi zinazolenga kuboresha ustawi wa jamii.

“Kama tunavyojivunia kuwa Mtandao wa Viwango, tunaamini viwango havipaswi kuishia kwenye huduma za mawasiliano pekee, bali vinapaswa kuonekana pia katika namna tunavyowajibika kwa jamii tunayoihudumia,” amesema.

Mutalemwa amesema Kampeni ya Tumaini ni endelevu na inatarajiwa kufika katika wilaya na mikoa mingine nchini baada ya kuanzia Dar es Salaam na sasa Ifakara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Pili Kitwana, amesema msaada huo utasaidia kupunguza upungufu wa baadhi ya vifaa muhimu vinavyotumika kutoa huduma za uzazi katika kituo hicho.

Amesema Kituo cha Afya Kibaoni kinahudumia idadi kubwa ya wananchi, hali inayoongeza mahitaji ya vifaa na miundombinu ya kutolea huduma, hivyo vifaa vilivyotolewa vinatarajiwa kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya kuwahudumia wajawazito na kina mama wanaofika kujifungua.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria makabidhiano hayo, akiwemo Diwani wa Kata ya Kibaoni, Rashidi Namtuka, wameeleza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wajawazito na kina mama wanaojifungua katika kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya (katikati), akiwaongoza wafanyakazi wa Yas Tanzania kukabidhi vifaa tiba na vifaa vya kujifungulia katika Kituo cha Afya Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro, hivi karibuni. Msaada huo ni sehemu ya Kampeni ya Tumaini inayoendeshwa na wafanyakazi wa Yas, yenye lengo la kuunga mkono huduma za afya ya mama kwa kutoa vifaa muhimu katika vituo vya afya nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...