Benki ya Absa Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Saaam waandaa Mkutano wa BEN-Africa wa Maadili ya Biashara Afrika
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa mwaka 2026 wa Mtandao wa Maadili ya Biashara Afrika (BEN-Africa), utakaofanyika Novemba 5 na 6 katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), ukiwaleta pamoja viongozi wa biashara, watunga sera, wasomi na wadau mbalimbali kujadili uongozi wenye maadili, utawala bora na mwenendo unaowajibika katika biashara.
Mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa Tanzania, BEN-Africa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Mitazamo Tofauti kuhusu Maadili ya Biashara: Mtazamo wa Kiafrika na Zaidi ya Hapo.”
Lengo la mkutano huo ni kuchunguza namna uongozi wenye maadili unavyoweza kuchangia maendeleo endelevu, kuimarisha uwajibikaji katika shughuli za biashara na kukuza ustawi wa muda mrefu wa bara la Afrika.
BEN-Africa, ambayo ni kifupi cha Business Ethics Network of Africa, ilianzishwa mwaka 1999 na imekua kuwa mtandao muhimu wa bara la Afrika unaowakutanisha wasomi, viongozi wa biashara, watunga sera na asasi za kiraia kujadili changamoto mbalimbali za kimaadili zinazolikabili bara hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Benki ya Absa Tanzania, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Sheria na Udhibiti, Alistides Kashasira, alisema maadili ni msingi muhimu wa kujenga taasisi endelevu, masoko yanayoaminika na jamii zenye ustawi.
“Maadili si suala la kutimiza tu matakwa ya uzingatiaji wa sheria na kanuni; bali ndiyo msingi unaojenga taasisi endelevu, masoko yanayoaminika na jamii zenye ustawi. Kama benki inayojivunia kuwa ya Kiafrika, Absa inaamini kuwa uongozi wenye maadili na utawala imara ni vichocheo muhimu vya ukuaji wa uchumi jumuishi,” alisema Kashasira.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa benki hiyo na BEN-Africa unaakisi dhamira yake ya kuendeleza uadilifu, uwajibikaji na mwenendo unaowajibika katika shughuli za biashara barani Afrika.
Ushirikiano huo pia unaendana na dhamira ya Absa Group ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamoja… hatua moja baada ya nyingine”, pamoja na juhudi zake za muda mrefu za kuimarisha utawala wenye maadili, uwazi na biashara jumuishi.
Kupitia udhamini wake wa BEN-Africa, Absa inalenga kuwezesha majadiliano yenye tija na ushirikiano katika kutafuta suluhisho yatakayosaidia kuimarisha utawala bora na maadili ya biashara barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga, alisema benki hiyo inajivunia kushirikiana na wadau kuileta BEN-Africa nchini Tanzania.
Alisema mkutano huo una maana kubwa zaidi ya udhamini, kwani unaakisi misingi ya benki hiyo na imani yake kwamba mwenendo wenye maadili, uongozi unaowajibika na uaminifu wa wadau ni nguzo muhimu za ukuaji endelevu.
Luhanga alisema mkutano huo pia utaipa Tanzania fursa ya kujitambulisha kama kitovu cha mijadala ya kitaalamu na mawazo bunifu, huku ukichochea majadiliano yatakayosaidia kuunda mustakabali wa biashara yenye maadili barani Afrika.
Programu ya mkutano huo itajumuisha hotuba kuu, mijadala ya majopo na majadiliano ya kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo mitazamo ya Kiafrika na Kimagharibi kuhusu maadili ya biashara, faida na mamlaka katika biashara, ukuaji endelevu wa uchumi na uongozi wenye maadili.
Mada nyingine zitakazojadiliwa ni ujasiriamali unaozingatia maadili, falsafa ya Kiafrika ya Ubuntu na akili unde (Artificial Intelligence — AI), utalii, utawala bora na mwenendo unaowajibika katika biashara, pamoja na wajibu wa kampuni kwa jamii na athari za shughuli zake kwa maendeleo ya kijamii.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika elimu ya juu na utafiti barani Afrika, kitakuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuchangia mijadala ya kitaaluma kuhusu maadili, uongozi na utawala bora.
Akizungumza kwa niaba ya chuo hicho, Dkt. Robert Suphian, Mkuu wa Idara ya Masoko na Kaimu Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema vyuo vikuu vina wajibu wa kuandaa si wahitimu wenye ujuzi pekee, bali pia viongozi wenye maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili jamii.
Alisema chuo hicho kina heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu na kuchangia juhudi za kuendeleza maadili, utawala bora na uongozi unaowajibika barani Afrika.
Mkutano wa mwaka 2026 utakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka wa BEN-Africa katika historia ya mtandao huo ya miaka 25, hatua inayoonesha nafasi inayoongezeka ya nchi katika mijadala ya kikanda kuhusu utawala bora, uongozi na maadili ya biashara.
Mkutano huo unatarajiwa kuvutia washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wakiwemo viongozi wa serikali, watendaji wakuu wa kampuni, wadhibiti, wasomi, watafiti, wanafunzi na wataalamu wa maendeleo.
BEN-Africa, Benki ya Absa Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vimewaalika wadau wote wanaojitolea kujenga Afrika yenye maadili, maendeleo endelevu na ustawi kushiriki katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu mkutano wa BEN-Africa 2026 unaohusu Maadili ya Biashara Afrika unaotarajiwa kufanyika Novemba 5 na 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Masoko na Kaimu Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Robert Suphian na kulia ni Mkurugenzi wa Sheria na Udhibiti wa Benki ya Absa Tanzania, Alistides Kashasira.
7688: Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga (wa tano kushoto), akipiga picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Masoko na Kaimu Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Robert Suphian (kulia), jijini Dar es Salaam leo, kuhusu mkutano wa BEN-Africa 2026 unaohusu Maadili ya Biashara Afrika unaotarajiwa kufanyika Novemba 5 na 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Wengine ni baadhi ya wafanyakazi kutoka Absa na wa UDSM.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...