Na Janeth Raphael - MichuziTv

Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza kuahirishwa kwa mashindano ya Rombo Marathon na Ndafu Festival yaliyokuwa yafanyike Desemba 23, 2026, katika Misitu ya Rungai, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, kutokana na tahadhari ya uwezekano wa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya hewa ya El Niño.

Akizungumza jijini Dodoma Oktoba 17, 2026, Prof. Mkenda amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano na bodi ya maandalizi ya matukio hayo, kwa kuzingatia usalama wa washiriki na wageni wanaotarajiwa kufika kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Amesema si busara kuendelea na maandalizi ya kuwapokea washiriki, ambao hutumia fedha na muda wao kushiriki katika matukio hayo, wakati kuna uwezekano wa kutokea kwa hali ya hewa inayoweza kuhatarisha usalama wao.

Prof. Mkenda amesisitiza kuwa licha ya kusikitishwa na kuahirishwa kwa matukio hayo, usalama wa watu ni kipaumbele kuliko kuendelea na shughuli hizo kwa sababu ya umaarufu wake. Ameongeza kuwa maandalizi yataendelea ili kuhakikisha Rombo Marathon na Ndafu Festival za mwaka 2027 zinafanyika kwa ukubwa zaidi.

Ameeleza kuwa matukio hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza utalii wa ndani, kutoa burudani kwa washiriki na familia zao, pamoja na kuitangaza Rombo kupitia mandhari ya Misitu ya Rungai na maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro. Aidha, yamekuwa yakivutia washiriki kutoka sehemu mbalimbali, wakiwemo viongozi na wanasiasa kutoka nchi jirani.

Kuhusu mchango wa kijamii, Prof. Mkenda amesema mapato yanayotokana na Rombo Marathon yamekuwa yakisaidia kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo miundombinu ya shule na huduma za afya katika Hospitali ya Huruma. Kwa upande wake, Ndafu Festival imeendelea kuwa jukwaa la kuvutia wageni na kuchochea utalii pamoja na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Amesema waandaaji wataendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu kuhusu hali ya hewa, huku akiwataka wadau na washiriki kuunga mkono maandalizi ya matukio hayo kwa mwaka 2027, yatakayolenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika miaka iliyopita.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...