NA DENIS MLOWE IRINGA 


SHIRIKA la Ilula Orphan Program (Tanzania) (IOP) limeeleza namna linavyotekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa lengo la kuboresha maisha ya jamii, hasa watoto, vijana, wanawake na wazee katika mikoa ya Iringa na wilaya ya Kilolo.

Akizungumza na wanahabari, MkurugenziMtendaji wa . Shirika hilo wakati wa maonesho ya Wiki ya NGOs, ambapo lilieleza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kupitia miradi yake ya kijamii pamoja na miradi ya kujitegemea inayolenga kuhakikisha huduma zinaendelea hata pale ufadhili kutoka kwa wahisani unapopungua.

Msigwa amesema kuwa miongoni mwa miradi ya kijamii inayotekelezwa ni kituo cha watoto kinachohudumia watoto 45, wakiwemo wasichana na wavulana, pamoja na mradi wa ufadhili wa elimu unaowezesha watoto kuanzia elimu ya awali hadi sekondari.

Shirika hilo limeeleza kuwa kupitia mradi huo linawahudumia watoto 616 katika ngazi mbalimbali za elimu, hatua inayolenga kuwawezesha kupata elimu na mazingira bora ya kujifunzia.

Aidha, IOP inaendesha mradi wa utoaji wa chakula cha mchana pamoja na msaada wa pembejeo za kilimo katika shule sita za msingi wilayani Kilolo.

"Lengo la mradi huo ni kuwawezesha watoto kupata mahitaji muhimu wakiwa shuleni, hususan wale wanaotoka katika maeneo ya mbali na shule na ambao hukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri mahudhurio na ujifunzaji wao." Alisema

Msigwa alisema kuwa katika eneo la kuwawezesha wasichana na akinamama waliopata ujauzito katika umri mdogo, IOP inaendesha programu inayolenga kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida na kutimiza ndoto zao ambazo zinaweza kuwa zimesitishwa kutokana na changamoto walizokutana nazo.

Ameongeza kuwa kwa sasa, shirika hilo lina akinamama sita wanaoishi katika nyumba maalumu huku wengine wakisaidiwa wakiwa majumbani kwao huku Programu hiyo inawahudumia wasichana na akinamama waliopata ujauzito katika umri mdogo, wakiwemo wenye umri wa miaka 14, 17 na 18, ambao wanakabiliwa na mazingira hatarishi.

Alisema kuwa katika mwaka wa kwanza wa programu hiyo, wanufaika hupatiwa mafunzo, msaada wa kisaikolojia pamoja na elimu ya malezi na makuzi ya watoto huku katika miaka inayofuata, wanajengewa uwezo katika fani mbalimbali kulingana na vipaji na mahitaji yao, huku baadhi wakichagua kurejea shuleni na wengine kujifunza ujuzi wa kuwawezesha kujitegemea.

Alisema kuwa shirika la IOP linaendesha mradi wa kuwawezesha wanawake na vijana katika wilaya za Iringa na Kilolo kwa kuwapatia fursa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kujenga maisha yao na upande wa wazee, shirika hilo linaendesha mradi unaowahudumia wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, ambapo kwa sasa linawafikia wazee 69.

Aliongeza kuwa IOP pia hufanya shughuli za utetezi kwa ajili ya wazee na kuwawezesha baadhi yao kupata bima za afya kulingana na mahitaji na hali zao ambapo mbali na miradi ya kijamii, IOP imesema imeanzisha miradi ya kujitegemea kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufadhili kutoka kwa wahisani ambao wakati mwingine unaweza kukoma bila taarifa ya kutosha.

Kutokana na hilo alisema kuwa kama IOP amekuwa na miradi ya kilimo, ambacho mbali na kuzalisha chakula kwa ajili ya shule na vituo vinavyomilikiwa na IOP, pia huzalisha mazao ya ziada yanayouzwa ili kupata mapato.

Shirika hilo pia linaendesha ufugaji wa kuku na uzalishaji wa maziwa, ambapo sehemu ya maziwa hutumika kulisha watoto wanaohudumiwa na IOP na sehemu nyingine huuzwa katika migahawa kwa ajili ya kupata mapato.

Aidha, IOP ina karakana inayohusika na utengenezaji wa samani kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuzwa nje, pamoja na kufanya ukarabati wa majengo ya shirika ,pia linaendesha taasisi za elimu zikiwemo shule ya awali, shule ya sekondari na chuo, ambazo ni sehemu ya juhudi zake za kuchangia maendeleo ya elimu na kujenga uwezo wa jamii.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...