Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala imepokea na kuridhia Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026, iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Jonas Mpogolo, huku ikitoa maazimio manane ya kuimarisha utekelezaji wa Ilani hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sultan Siddem, amemshukuru Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema imegusa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ilala na kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Akisoma maazimio hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Jesca Msangi, amesema azimio la kwanza ni kumpongeza Rais Dk. Samia kwa utendaji kazi, uongozi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Amesema azimio la pili ni kuwapongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Charangwa Selemani, kwa kuaminiwa na Rais Dk. Samia kuendelea kuwahudumia wananchi wa Ilala.
“Azimio la tatu ni kwamba Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala imepokea Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani, maoni na ushauri wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, ambayo ilifanya ziara ya ukaguzi wa miradi na imeridhishwa na kazi kubwa ya utekelezaji iliyofanywa na usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mpogolo,” amesema Jesca.
Amesema azimio la nne ni kuhimiza utunzaji wa miradi yote ya maendeleo iliyotekelezwa, ikiwemo barabara, ili kuzuia uharibifu wake muda mfupi baada ya kuanza kutumika.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi hiyo, hivyo wananchi na viongozi wanapaswa kuwa na elimu ya uzalendo na kutambua umuhimu wa kutunza miundombinu iliyojengwa katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Jesca, azimio la tano ni kusisitiza kuwepo kwa mipango madhubuti ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño, ikiwemo kukamilisha kwa wakati miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na mitaro, kusafisha mifereji, kuzoa taka na kuwaelimisha wananchi, hasa wanaoishi maeneo hatarishi na mabondeni, kuchukua tahadhari.
Azimio la sita ni kuitaka Serikali kukamilisha mchakato wa kufuta hati ya eneo la Kabimita, Mtaa wa Banguro, ili kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi yao kihalali.
Azimio la saba ni kuwapongeza wabunge na madiwani wote wa CCM kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama, huku azimio la nane likisisitiza Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, kama chombo kikuu cha utekelezaji wa Ilani kwa mujibu wa Katiba ya Chama, kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kukagua, kutoa ushauri na maelekezo, kutoa msukumo pamoja na kuutangaza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali kwa wananchi.
DC MPOGOLO
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mafanikio yaliyopatikana yanatokana na maono ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miradi ya maendeleo.
Amesema moja ya maeneo ya kipaumbele ni maandalizi ya kupokea ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, maarufu kama Double Cohort.
ELIMU
Mpogolo amesema Wilaya ya Ilala imetenga Sh bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wapatao 85,000 watakaojiunga na kidato cha kwanza.
Amesema wilaya hiyo inaendelea na ujenzi wa shule za sekondari zenye majengo ya ghorofa, upatikanaji wa vifaa vya elimu pamoja na kuunda kamati maalumu itakayoratibu na kusimamia maandalizi hayo.
EL NIÑO
Kuhusu maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño, Mpogolo amesema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa, ikiwemo kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko, kuzibua mitaro na mifereji pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua wakati wa mvua.
“Tunataka kuhakikisha barabara zote zinazojengwa pamoja na madaraja vinakamilika kabla ya mvua hiyo kuanza kunyesha, likiwemo Daraja la Segerea–Majumba Sita na Daraja la Bonyokwa, ambayo yako katika hatua za mwisho za kukamilika,” amesema.
Amesema hatua za kukabiliana na El Niño zinahusisha maandalizi kabla, wakati na baada ya mvua, huku Jiji la Dar es Salaam likishirikiana na taasisi, wadau na makundi mbalimbali katika kuokoa watu na mali zao.
Amesema pia maeneo na vituo maalumu vinaandaliwa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za afya kwa waathirika wa mafuriko.
Mpogolo amesema Jiji la Dar es Salaam tayari limetenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, huku akiwataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi, hususan mabondeni, kuhama mapema.
USAFI
Akizungumzia suala la usafi, Mpogolo amesema Wilaya ya Ilala imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dk. Samia pamoja na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kwa kulipa uzito mkubwa ajenda ya usafi.
Amesema pamoja na kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi na wadau, wilaya imeboresha njia za kuingia na kutoka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi na kuwapa wakandarasi wa uzoaji taka muda wa miezi mitatu kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kisasa vya kufanyia usafi.
Amesema pia usimamizi wa sheria ndogo za usafi umeimarishwa kupitia kikosi maalumu kinachojumuisha vijana waliopata mafunzo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Akiba pamoja na wataalamu wa mazingira.
Kikosi hicho kina jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria za usafi, kuwakamata wanaokiuka sheria, kuwatoza faini na kuwafikisha mahakamani pale inapobidi.
“Lengo ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi na wananchi wanajenga utamaduni wa kuwa wasafi wakati wote,” amesema.
UWEZESHAJI WANANCHI
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 2.4 kwa vikundi vya wajasiriamali, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Amesema Sh bilioni 22 zipo katika akaunti zikisubiri kukopeshwa kwa walengwa.
“Pia Halmashauri imetenga Sh bilioni 6.4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuwawezesha wajasiriamali, hususan wanaonufaika na fedha hizi. Katika Kata ya Pugu tunajenga Kituo Atamizi cha Wajasiriamali, ambacho ujenzi wake unagharimu Sh milioni 990.4, kitakachosaidia kutoa mafunzo kwa wajasiriamali hao na kuongeza thamani ya bidhaa zao,” amesema.
MAPATO
Akizungumzia suala la mapato, Mpogolo amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwezesha kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miaka minne, ambapo amesema mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 81 hadi kufikia Sh bilioni 171.
“Hii ndiyo siri ya ufanisi wa utekelezaji wa Ilani hii. Tunamshukuru Rais Dk. Samia, alipoingia madarakani alitupa utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa mapato,” amesema.
Amesema Wilaya ya Ilala na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zimejipanga kuendelea na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, huku akiwashukuru viongozi wa CCM Wilaya ya Ilala kwa usimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...