Na Mwandishi Wetu, Kilwa

MAMBO makubwa matatu ya kimkakati yametekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuwezesha eneo lenye utajiri wa historia ya namna vita vya Majimaji ilivyoanza kupiganwa Julai 15, 1905 katika vijiji vya Nandete na Kibata, Kata ya Kipatimu, wilayani Kilwa mkoani Lindi yanaingizwa kwenye orodha ya maeneo yaliyo katika Urithi wa Dunia.

Tayari eneo hilo muhimu lenye kumbukumbu kadhaa ikiwemo mche wa pamba, zao ambalo ndilo lilikuwa chanzo cha kuanza kwa vita hivyo, mapango yaliyotumika kujificha, nyumba za asili za kabila la Wamatumbi, Boma aliloishi Mjerumani na kisima cha maji alichotumia Mjerumani yameingizwa kwenye orodha ya Urithi wa Taifa.

Utekelezaji wa mambo hayo matatu ya kimkakati umetajwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Malikale katika Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita wakati akitoa salamu za Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 121 ya Kuanza kwa Vita vya Majimaji yaliyofanyika katika Kijiji cha Nandete juzi.

Mambo yaliyotekelezwa kwa kiwango cha juu na Wizara ya Maliasili na Utalii hadi sasa ni pamoja na kuanza kuandikwa upya kwa historia ya kuanza kwa vita hivyo ili kueleza kwa ufasaha mahali, sababu na namna vita hivyo vilivyoanza na kupiganwa katika eneo hilo la Nandete kabla ya kusambaa nchi nzima na kuhitimishwa mkoani Ruvuma.

Baada ya kuanza katika eneo hilo la Nandete mkoani Lindi baada ya Wamatumbi kupinga unyanyasi uliokuwa unafanywa na Utawala wa Mjerumani kwa kuwatumikisha katika mashamba ya pamba, vita hivyo vilisambaa katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa na hatimaye Ruvuma ilikotamatika Agosti 8, 1907.

Jambo la pili la kimkakati lililotekelezwa ni kuanza kufungamanisha mnyororo mzima wa maeneo ambayo vita hivyo vilipiganwa kwa kuanzisha maadhimisho ya kumbukizi kwa lengo la kuenzi tunu na ushujaa uliofanywa na wazee wa maeneo hayo katika kulipigania Taifa lao kama sehemu ya kuamsha ujasiri, umoja, mshikamo na uzalendo kwa vizazi vya sasa katika kulilinda Taifa lao kwa wivu mkubwa.

Jambo la tatu ambalo pia limetekelezwa kwa ufanisi mkubwa ni ujenzi wa Kituo cha Kukusanya taarifa kuhusu Kuanza kwa Vita vya Majimaji kilichopo katika Kijiji cha Nandete ambapo serikali imetoa takribani Sh bilioni 1.3 ili kugharamia ujenzi wake, kikitarajiwa kukamilika na kuanza kutumika mapema mwaka 2027.

Mkurugenzi Msaidizi Mwita anasema hatua hiyo mbali ya kuwezesha eneo hilo kutambuliwa kama sehemu ya urithi wa dunia, kukamilika kwa program hizo zinazoendelea kuchukuliwa kutawezesha pia kukuza utalii katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, kukuza ajira, kuinua uchumi wa nchi, kujenga Taifa la vijana wanaojua nchi imetoka wapi na inakokwenda na hivyo kujenga uzalendo, umoja na mshikamano wa kitaifa.







Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...