-Baada ya Miaka 15 ya Utumishi, Louis-Olivier Favot Mkurugenzi Mtendaji Mpya

Mixx Tanzania imetangaza mabadiliko katika uongozi wake wa juu, huku Angelica Pesha akihitimisha safari yake ya zaidi ya miaka 15 katika kampuni hiyo na Louis-Olivier Favot akiteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya.

Mabadiliko hayo yanaashiria mwisho wa safari ndefu ya Pesha katika kuijenga na kuiendeleza kampuni, tangu ilipoanza kama Tigo Pesa hadi kuwa kampuni kubwa ya teknolojia ya fedha (fintech) inayotoa huduma mbalimbali za kifedha kidijitali nchini Tanzania.

Wakati huo huo, Mixx Tanzania imemteua Favot, kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika huduma za benki, huduma ndogo za fedha, fedha kwa njia ya simu na huduma nyingine za kifedha za kidijitali

Miaka 15 ya Angelica Pesha: Kutoka Tigo Pesa hadi Mixx Tanzania

Safari ya Pesha ilianza katika siku za mwanzo za Tigo Pesa, wakati huduma za fedha kwa njia ya simu zilipoanza kubadili namna Watanzania wanavyotuma, kupokea na kusimamia fedha zao.

Kwa zaidi ya miaka 15, Pesha amekuwa na mchango mkubwa katika safari ya taasisi hiyo, kutoka kuwa huduma ya fedha kwa njia ya simu ndani ya Tigo hadi kuwa kampuni kinara ya teknolojia ya fedha inayotoa huduma mbalimbali za fedha mtandao.

Katika kipindi chake cha uongozi, Pesha alishiriki katika kuanzisha na kuendeleza huduma mbalimbali za ubunifu, zikiwemo kuunganisha huduma za fedha kwa njia ya simu kati ya mitandao mbalimbali, uhamishaji wa fedha ndani na nje ya nchi, Applikesheni ya Tigo Pesa, kuunganisha huduma za benki na kampuni za simu, kupokea fedha kutoka nje ya nchi, malipo, akiba na mikopo ya kidijitali.

Safari hiyo ilienda sambamba na mabadiliko makubwa katika sekta ya huduma za kifedha nchini, huku teknolojia ya simu za mkononi ikongeza ujumuishwaji wa kifedha kwa mamilioni ya Watanzania.

Pesha aliteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu mwaka 2020 na baadaye akaongoza kampuni katika kipindi muhimu cha mabadiliko kutoka Tigo Pesa hadi Mixx Tanzania. Katika kipindi hicho, alisimamia pia uimarishaji wa mifumo ya utawala, teknolojia, taratibu za kazi, miundo ya uongozi na uwezo wa wafanyakazi.

Chini ya uongozi wake, Mixx iliendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza huduma za kifedha za kidijitali nchini, na kutambuliwa kwa mafanikio hayo kupitia tuzo mbalimbali za ubora na ubunifu. Miongoni mwa tuzo hizo ni tuzo tatu ilizopokea katika Tuzo za TEHAMA mwezi Agosti 2026, zikiwemo Tuzo ya Ubunifu katika Huduma za Fedha kwa Njia ya Simu huku Pesha alitunukiwa Tuzo ya Uongozi wa Kike katika TEHAMA.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Erwan Gelebart, Mkurugenzi Mtendaji wa AXIAN Digibank & Fintech, alimshukuru Pesha kwa uongozi mahiri na mchango wake katika ukuaji wa Mixx kitaasisi, maendeleo endelevu na utekelezaji wa mikakati ya kampuni.

“Angelica amekuwa sehemu muhimu ya safari ya Mixx Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, yeye pamoja na timu yake wameijenga biashara hii kutoka mwanzo hadi kuwa kampuni kubwa na mshirika anayeaminika katika maisha ya kila siku ya Watanzania,” alisema Gelebart.

Aidha alisema kuwa mchango wa Pesha haukuishia katika mafanikio ya kibiashara, bali ulihusisha pia kujenga, kuongoza na kuwawezesha watu na timu alizofanya nazo kazi.

Louis-Olivier Favot Awa Afisa Mtendaji Mkuu Mpya

Favot anajiunga na Mixx Tanzania akiwa na uzoefu wa miaka 17 katika sekta za benki, huduma ndogo za fedha, huduma za fedha kwa njia ya simu na huduma za kifedha za kidijitali. Kati ya hiyo, miaka 14 amefanya kazi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Uzoefu wake unahusisha kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha, kubuni bidhaa, kuendesha biashara, kuboresha uzoefu wa wateja, kusimamia utoaji wa huduma na kutumia teknolojia kuboresha mifumo na huduma.

Kabla ya kujiunga na Mixx Tanzania, Favot alikuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji na baadaye Afisa Mtendaji Mkuu wa MVola, kampuni tanzu ya AXIAN inayotoa huduma za kifedha za kidijitali nchini Madagascar.

Alijiunga na MVola mwaka 2020 kama Mkurugenzi wa Uendeshaji, akisimamia shughuli za kila siku za kampuni pamoja na maendeleo na utoaji wa huduma za kifedha za kidijitali.

Uzoefu huo unamweka Favot katika nafasi nzuri ya kuongoza awamu inayofuata ya ukuaji wa Mixx Tanzania, huku akisaidia kupanua zaidi upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania.

Uteuzi wake unafanyika wakati Mixx ikiendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya huduma za kifedha za kidijitali, ikitoa huduma za malipo na suluhisho mbalimbali za kifedha kwa watu binafsi, wafanyabiashara na kampuni.

Akizungumza kuhusu uteuzi huo, Gelebart alimkaribisha Favot Mixx Tanzania na kumtakia mafanikio katika nafasi yake hiyo mpya.

“Louis-Olivier, karibu sana Mixx Tanzania! Nakutakia kila laheri na mafanikio katika nafasi yako mpya.”

Mabadiliko haya ya uongozi yanafanyika wakati Mixx Tanzania ikiendelea kutekeleza azma yake ya kutoa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, bunifu na zinazotumia teknolojia ya kidijitali kurahisisha upatikanaji hudum kwa gharama nafuu.


Louis-Olivier Favot - Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mixx Tanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...