Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, amewahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa za uwekezaji na umiliki wa mali wakiwa katika umri mdogo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uhuru wa kiuchumi na kuimarisha maisha yao ya baadaye.
Juneid alitoa wito huo katika kongamano la wanawake la Women in Diplomacy Power Table, lililoandaliwa na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, ambapo alisisitiza kuwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi una manufaa si kwa familia pekee, bali pia kwa jamii nzima.
Alisema baadhi ya mitazamo na mila za kijamii zimekuwa kikwazo kwa wanawake kumiliki mali, hususan ardhi na nyumba, hivyo akasisitiza umuhimu wa kubadili fikra hizo na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za uwekezaji.
Alieleza kuwa Mkuyu Africa, kupitia mpango wake wa Miliki Mali, inalenga kuwawezesha wanawake na vijana kumiliki nyumba na viwanja kwa utaratibu unaorahisisha upatikanaji wa mali hizo.
“Nyumba inaweza kuwa na ghorofa 10, lakini unaweza kununua na kumiliki sehemu ya jengo hilo kulingana na utaratibu wa mradi. Utapatiwa nyaraka za umiliki zinazotambulika kisheria zitakazokuwezesha kuitumia mali hiyo kwa kuishi au kuipangisha,” alisema Juneid.
Kwa upande wake, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, ameitaka jamii kuimarisha mapambano dhidi ya ndoa za utotoni na kuongeza uwekezaji katika elimu na haki za wasichana.
Akizungumza katika kongamano hilo lililobeba kaulimbiu ya “Nguvu ya Mtoto wa Kike: Komesha Ndoa za Utotoni, Wekeza katika Haki za Wasichana,” Mulamula alisema ndoa za utotoni huwanyima wasichana fursa za elimu na uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wa maisha yao.
Alisisitiza kuwa kulinda haki za mtoto wa kike ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa Serikali, wazazi, viongozi wa jamii, wanadiplomasia na sekta binafsi.
Mulamula aliongeza kuwa wanaume na wavulana wanapaswa kushirikishwa katika juhudi hizo ili kuhakikisha wasichana wanapata mazingira salama ya kujifunza, kukuza vipaji na kutimiza ndoto zao.
Alisema uwekezaji katika elimu na haki za wasichana ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya mataifa.
Naye Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, alisema kongamano hilo limelenga kuhamasisha wanawake na vijana kujiamini, kujituma na kutumia fursa za uwekezaji ili kuimarisha uwezo wao wa kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, aliwahimiza kutumia mitandao ya kijamii kwa tija, ikiwamo kujifunza na kutafuta fursa za kujipatia kipato kupitia majukwaa hayo.
Mkurugezi wa Mkuyu Africa Juneid Othman akizungumza wakati wa kongamano la wanawake la( Women in Diplomacy Power Table) lilofanyika jijini Dar es salaam


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...