Na Janeth Raphael - MichuziTv


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida, huku akiwataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Msigwa amesisitiza kuwa malengo ya maendeleo hayawezi kufikiwa iwapo wananchi watahamasishana kushiriki katika vitendo vinavyovunja amani, akibainisha kuwa madai na changamoto zinazowakabili wananchi zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za amani badala ya kutumia vurugu.

Akizungumza leo jijini Dodoma, eneo la Mtumba, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Msigwa amesema wananchi wanapaswa kujiepusha na migogoro na vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi, kwa kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo.

Ameeleza kuwa matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana ni somo kwa Watanzania, akisema baadhi ya watu waliohamasisha vurugu hizo walikimbia na kuiacha Serikali ikikabiliana na jukumu la kurejesha na kuimarisha amani.

Msigwa amesisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba kila anayekiuka sheria anapaswa kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha, amewataka vijana, ambao ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, kuepuka kutumiwa vibaya katika shughuli zinazoweza kuhatarisha amani na badala yake kutumia majukwaa hayo kama fursa za kujifunza, kufanya biashara na kujipatia kipato.

Amesema matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwasaidia vijana kujenga fursa za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa, badala ya kushiriki katika shughuli zinazoweza kuleta migogoro na kuvuruga utulivu wa nchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...