MKAZI wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Monica Mujungu ameliomba Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kinondoni kutenda haki kwani wakili wa mpinzani wake, Benjamin Karume anatumia taaluma yake ya Sheri kuishawishi mahakama imnyime haki yake.
Monica alidai hayo mbele ya Hakimu Joaquine Cheng'a wakati pingamizi alilowasilisha kwamba anayemdai gharama za kesi takribani Sh milioni 10 hajawahi kushtakiana naye mahakamani likisikilizwa.
Monica aliwasilisha pingamizi dhidi ya Adon Christian Hajayandi akidai hajawahi kushtakiana naye mahakamani, aliyeshtakiana naye ni Hajayandi Adon.
Wakili wa Hajayandi, Benjamin Karume alidai mteja wake aliwahi kufunguliwa kesi ya mgogoro wa mpaka katika eneo lililopo Kimara Temboni na Monica iliyosikilizwa upande mmoja na kumpa ushindi Monica .
Alidai aliwasilisha maombi ya kutengua hukumu hiyo na ilitenguliwa Septemba 3, 2021 na akaamuliwa Monica kuwasilisha maombi mengine.
Wakili Karume alidai aliwasilisha maombi mapya Mei 25,2026 Ili upande wao wawasilishe majibu ya utetezi,
majina yakiwa Monica Kalibona Mujungu dhidi ya Adon Christian Hajayandi, shauri hilo pia likafutwa Julai 2 mwaka huu kwa gharama.
"Mheshimiwa akisema hajafanya kesi na Adon ni kujichanganya mwenyewe, hoja haina mashiko tuendelee na shauri la gharama za kesi,"anadai Wakili Karume.
Akijibu Monica anadai hajawahi kuwasikisha maombi ya Mei mwaka huu dhidi ya Adon na kwamba kesi iliisha mwaka 2021.
"Mheshimiwa Wakili anatumia ujuzi wake kuishawishi Mahakama kwa sababu kesi iliisha 2021 na hukumu ipo, nilikazia hukumu na kukabidhiwa eneo.
"Mwaka 2022 alifaili kesi namba 130, alidai kesi ilisikilizwa upande mmoja, hajahudhuria ikafutwa, alidai ni mfanyakazi wa Ikulu alihamishwa mkoa, akaomba kesi ianze upya.
"Wakati huo Baraza la Ardhi Ubungo lilishaanza nikaomba kesi yangu ihamie huko Hakimu aliyekuwa akisikiliza awali alinikatalia.
"Kesi iliendeshwa kwa jina la Hajayandi Adon, mwanzoni nilimfahamu kwa jina la Adon Christian Hajayandi, nilipompelekea hati ya wito wa mahakama alikataa akidai si jina lake, alidai jina lake sahihi ni Hajayandi Adon,"anadai Monica na kuongezea kwamba hata kesi alizowasilisha aliandika Hajayandi Adon
"Anachokifanya ni kutaka kunisumbua, naomba mahakama itambue anatumia ujuzi wake kuninyanyasa, kesi tulifanya na Hajayandi Adon sio Adon Christian Hajayandi, naomba maombi yake ya gharama yatupiliwe mbali.
"Alipewa ushindi ambao sielewi, naomba nipate haki yangu, kesi itupiliwe mbali, niliyowasilisha isikilizwe,"anadai Monica.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...